WIZARA YA MALIASILI YAZIDI KUNG’ARA, YAVUKA HATUA YA MAKUNDI MCHEZO WA KAMBA MEI MOSI ARUSHA

0

Na. John I. Bera – Arusha.

Timu za Kamba za Wizara ya Maliasili na Utalii zimeibuka mshindi kwenye mchezo wa kamba uliochezwa mapema leo ambapo timu ya Wanawake imeibuka mshindi kwa seti mbili kwa nunge dhidi ya timu ya Wizara ya Maji huku Wanaume wakiibuka na ushindi wa seti 2 kwa 1 dhidi ya hasimu wao Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwenye Mashindano ya Mei Mosi 2024 yanayoendelea kufanyika Jijini Arusha

Akizungumza mara baada ya ushindi huo, Kapteni wa kamba kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Sharifa Dunia amesema ushindi walioupata umetokana na mazoezi na maandalizi mazuri waliyoyafanya awali.

“Nawashukuru wachezaji wenzangu kwa jitihada zao, nidhamu pamoja na utii mazoezini, kwa uwezo wa MUNGU tumeweza kuwafunga seti zote mbili” amesema Sharifa.

Aidha, ameuahidi uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwamba yeye pamoja na wachezaji wenzake watahakikisha wanafanya vizuri mpaka mwisho na kurudi na vikombe huku akisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kutangaza utalii.

Kwa upande wa Kapteni Msaidizi wa Timu ya Kamba kwa Wanaume, Bw. Jumanne Ally amesema ushindi walioupata umetokana na jitihada za kila mchezaji hasa katika mazoezi ikiwemo kufuata maelekezo wanayopewa na mwalimu pindi wanapofanya mazoezi hayo.

Aidha ameongeza kuwa mbinu walizojifunza pindi wanapofanya mazoezi zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wanamshinda mpinzani wao.

Sambamba na hayo, Siku ya leo Mashindano yameendelea ambapo upande wa mashindano ya riadha yalifanyika ambapo kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii mwanariadha Athumani Simbiri ameingia fainali kwenye mbio za mita 200, Elibariki Buko ameendelea kutikisa kwa kushika nafasi ya 3 kwenye mbio za mita 1500, Saing’ati Kispan yeye alishika nafasi ya 3 mbio za mita 800, Bertha Chalamila ametinga nusu fainali ya mita 200, na hivyo kuiletea Wizara ushindi

Aidha, wengine walioshindana ni pamoja na, Julian Kaswahili ambaye ameshika nafasi ya 4 kwenye mbio za mita 400 na 800, Jehovaness Sarakikye nafasi ya nne mbio za mita 1500.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *