AJITEKA BAADA YA KULIWA MILIONI 200 KWENYE MCHEZO WA KUBETI
Mwanaume mwenye umri wa miaka 25, Nobert Mulwo ameshtua Familia yake na Maafisa wa upelelezi Nchini Kenya baada ya kubainika kuwa alijiteka na akajijeruhi kisha kudai fidia ya Ksh. 100,000 (takribani mil 1 na laki 8 za Kitanzania) ili kufidia mshahara wake wa Novemba alioupoteza kwenye kubeti.
Kwa mujibu wa CitizenTv Kenya, Familia ya Mulwo iliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kajiado ikidai kuwa alitekwa nyara na Watu wasiojulikana waliokuwa wakitumia Gari aina ya Toyota Probox huko Kitengela usiku wa Alhamisi na baadaye Watekaji walituma ujumbe kwa Dada yake Mulwo wakidai kiasi hicho cha pesa kama fidia ya kumwachia huru.
Kwa lengo la kufanya madai yake yaonekane ya kweli Mulwo alijijeruhi kwa kutumia wembe akajifunga kwa kamba mikononi na miguuni na kufunga mdomo wake kwa bandeji zenye damu kisha akatuma picha za hali hiyo kwa Dada yake kama ushahidi wa ukatili wa Watekaji wake.
Hata hivyo Maafisa wa upelelezi walifuatilia na kumkuta Mulwo akiwa katika Nyumba ya kulala Wageni ya Mutuku Lodgings pia walibaini kuwa Mulwo mwenyewe ndiye aliyepanga njama hiyo kwa kushirikiana na Mshirika wake anayejulikana kwa Jina moja tu Ndolo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wapelelezi vitu vilivyokamatwa ni pamoja na shilingi za Kenya elfu 10,100,Simu aliyotumia kuwasiliana na Familia yake, Wembe aliotumia kujijeruhi na bandeji na sasa Mulwo anashikiliwa akisubiri kufikishwa Mahakamani.