UJENZI WA MAJENGO YA WIZARA DODOMA WAKAMILIKA KWA 90%, NHC YAWEKA REKODI YA UBORA
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limefikia hatua ya mwisho katika kukamilisha ujenzi wa majengo ya kisasa kwa ajili ya ofisi za wizara mbalimbali za Serikali katika Mji wa Serikali jijini Dodoma. Ujenzi wa majengo haya umefikia asilimia 90, huku kazi zilizobakia zikiendelea kwa kasi ili kuhakikisha yanakamilika kwa wakati na kwa viwango vya hali ya juu.
Majengo haya ya wizara nane ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha miundombinu na huduma kwa ajili ya watumishi wa umma. Wizara zinazojengewa ofisi hizi ni pamoja na:
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini, Wizara ya Viwanda na Biashara.
Kazi zilizobaki ni pamoja na:Ufungaji wa vifaa vya zimamoto katika awamu ya mwisho, Ufungaji wa vifaa vya TEHAMA, Uwekaji wa taa kwenye majengo na maeneo ya nje (landscape lighting)
Majengo haya yamejengwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa na vimezingatia mahitaji ya utendaji wa wizara husika. Ujenzi wa majengo ya wizara hizi ni sehemu ya dhamira ya NHC kuhakikisha kuwa Serikali inapata ofisi bora, salama, na za kisasa ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Shirika la Nyumba la Taifa linaendelea kuthibitisha uwezo wake kama mdau muhimu katika maendeleo ya miundombinu ya kitaifa. Kukamilika kwa majengo haya kutaleta taswira mpya kwa Mji wa Serikali jijini Dodoma na kuimarisha mazingira ya kazi kwa wizara hizi muhimu.