MAKONDA NA BALOZI WA INDIA NCHINI BISHWADIP WEY WAJA NA FURSA ZA KIUCHUMI

0

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda leo Alhamisi Machi 13, 2025, amekutana na kuzungumza na Balozi wa India nchini Tanzania Mhe. Bishwadip Wey, wakikubaliana kukuza na kuimarisha mahusiano ya pande hizo mbili katika kuhakikisha kuwa wananchi wa Arusha wananufaika na fursa mbalimbali kutoka nchini India.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Makonda na Balozi Wey wamejadiliana na Mkoa wa Arusha kupata fursa ya mambo matano ikiwemo, Kongamano kubwa litakalofanyika Mwezi Mei mwaka huu, ambapo atakuwepo Profesa nguli kutoka nchini Marekani kutoa elimu kuhusu akili mnemba (Artificial Inteligence) kwa vijana wa Arusha.

Aidha, wamejadiliana kuanzisha mahusiano na Chuo cha Zanzibar kinachofadhiliwa na serikali ya India, katika kushirikiana pamoja na mkoa wa Arusha katika matumizi ya Teknolojia ya Akili mnemba katika utendaji wa kazi.

Viongozi hao pia katika mazungumzo yao wamekubaliana kuanzisha kilimo cha mitishamba inayotumika katika utengenezaji wa dawa za asili chini ya usimamizi wa Chuo kikuu cha Nelson Mandela.

Pia wamejadili kuhusu nchi ya India kutoa fursa za ufadhili wa masomo kwa vijana takribani 1000 watakaokuwa na fursa za kusoma kozi mbalimbali sambamba na ufadhili wa wapishi 50 watakaoenda kupata mafunzo ya upishi wa vyakula vyenye ladha ya kihindi ili kuvutia watalii kutoka nchini humo watakaokuja Tanzania.

Fursa nyingine iliyopatikana katika mazungumzo ya Mhe. Makonda na Balozi huyo wa India nchini Tanzania ni pamoja na kuimarisha kilimo cha maembe mkoani Arusha kutokana na uhakika wa soko linalopatikana nchini India, ambapo raia wa nchi hiyo wamekuwa na uhitaji mkubwa wa Unga unaotokana na tunda la embe kwaajili ya matumizi mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *