SALIM ASAS AKABIDHI GARI JIPYA KWA JESHI LA POLISI MKOA WA IRINGA

Katika kuhakikisha ajali za mara kwa mara na matukio ya kihalifu barabarani yanathibitiwa kwa kiasi kikubwa, Kamati ya Ulinzi na Usalama Barabarani mkoa wa Iringa Chini ya Mwenyekiti wake Mnec Salim Abri Asas imetoa gari mpya aina ya Land Cruizer Hilux Double Cabin yenye thamani ya Shilingi Milioni 100 kwa Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani mkoa wa lringa.
Gari hilo limekabidhiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani mkoa wa Iringa, Salim Abri Asas katika hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika Mjini Iringa.


Mnec Asas amesema upatikani wa Gari hilo litapunguza changamoto mbalimbali za barabarani hivyo gari hilo la kisasa litasaidia kuimarisha doria kwa jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani na kazi nyingine za jeshi hilo.
“ sasa hivi tuna idadi nyingi ya Vyombo vya moto kwa maana ya magari , pikipiki , bajaji na usafiri mingine hivyo tunahitaji vitendea kazi zaidi ili udhibiti na usimamizi vifanyike kwa hali ya juu kabisa “ Amesema Mnec Asas
Vile vile Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa SACP Allan Bukumbi amesema gari hilo litatumika ipasavyo na amemshukuru pia Mwenyekiti wa kamati hiyo Salim Abri hasa kwa mchango wake mkubwa kuhusu usalama barabarani na Mkoa wa Iringa kwa Ujumla.