RC SHINYANGA AAGIZA USHIRIKIANO NA COPRA KWENYE BIASHARA YA CHOROKO
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amesema serikali mkoani Shinyanga itashirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) na taasisi zote zinazosimamia Mwongozo wa biashara wa Mazao ya Dengu, Choroko, mbaazi, soya na ufuta ili kuhakikisha biashara ya Mazao hayo inafanyika rasmi na kwa usawa kwa wadau wote wa Mazao hayo.

Mhe. Macha ameyasema hayo kwenye kikao cha wadau wa Mazao ya choroko na dengu kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Manispaa ya Shinyanga.
Mhe. Macha amewaagiza wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri kushirikiana kwa karibu na COPRA, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) kuhakikisha biashara ya zao la choroko inafanyika kwa mafanikio katika mkoa wa Shinyanga kwa kufuata Mwongozo uliotolewa.
Awali akiwasilisha Mwongozo wa biashara ya mazao ya ufuta, choroko, mbaazi, dengu na soya Mkurugenzi Mkuu wa COPRA Bi. Irene Mlola amesema wakulima watakapouza mazao yao kwa kufuata mifumo ya biashara iliyowekwa ikiwemo minada ya kidigitali na kutumia stakabadhi ya ghala watafanya biashara kwa haki na uwazi kwani mkulima atakuwa huru kufuatilia mauzo ya Mazao yake akiwa katika kituo maalum au ghala lenye Mazao kupitia runinga au kiunganishi ambapo ataweza kuona wanunuzi wakishindana kununua mzigo wake.

Mkurugenzi Mlola amesema uwazi huo utampa mkulima au mkusanyaji mazao fursa kuuza mazao yake kwa bei ambayo itampa maslahi na endapo bei haitakuwa ya maslahi mweka mali anaweza kusitisha kuuza Mazao yake.
Aidha Mkurugenzi Mlola amesisitiza kuwa vipimo rasmi vinavyotambuliwa na wakala wa vipimo vitatumika kupima mali ya wakulima ili biashara ifanyike kwa haki na hatimaye mkulima atapata haki yake kwani hakutakuwa na nafasi ya kufanyika udanganyifu wowote ambao utasababisha dhuluma kwa wakulima.
