Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeendelea na zoezi lake la ukaguzi wa mita kwa wateja wa umeme ili kuwabaini wanaojihusisha na wizi wa umeme.
Zoezi hilo limefanyika tarehe 02 Februari, 2026 jijini Dodoma likiongozwa na timu ya wataalamu mbalimbali wakiwemo wahandisi, maafisa usalama pamoja na mafundi umeme kutoka TANESCO.
Katika ukaguzi huo, TANESCO imefanikiwa kubaini wateja kadhaa waliokuwa wakitumia umeme kinyume cha sheria, ambapo mita mbili zimekutwa zimehamishwa kiholela bila kufuata taratibu zilizowekwa. Miongoni mwao, mteja mmoja alibainika kufanya kuchepusha umeme kwenye mita yake, huku mwingine akitumia umeme kwa kipindi cha takribani miaka miwili bila kulipa gharama zozote.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Mapato TANESCO, Mhandisi Mposheleye Mwasenga, ameeleza kuwa Shirika hilo linaendelea kutoa wito kwa wananchi na wateja wote wa umeme kuzingatia matumizi halali ya umeme.
“Tunawasihi wananchi na wateja kwa ujumla wanunue umeme kulingana na matumizi yao halisi na waepuke kutumia njia zisizo sahihi, kwani hatua hizo husababisha gharama zisizo za lazima pamoja na adhabu kali,” amesema Mwasenga.
TANESCO imesisitiza kuwa itaendelea na zoezi la ukaguzi katika maeneo mbalimbali nchini kama sehemu ya kudhibiti upotevu wa mapato na kuhakikisha matumizi salama na halali ya umeme.