Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati Dodoma, Coster Osmund Mpagike, akiwa ameambatana na baadhi ya wafanyakazi wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha PSSSF, ametembelea ofisi za Makao Makuu ya Uhondo Media zilizopo Makole, jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo, kiongozi huyo pamoja na wafanyakazi aliokuwa nao walipata fursa ya kufanya mazungumzo na baadhi ya wafanyakazi wa Uhondo Media, ambapo walijadili masuala mbalimbali yenye lengo la kuimarisha ushirikiano na mshikamano kati ya taasisi hizo mbili.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kuboresha mahusiano ya kikazi na kuimarisha ushirikiano utakaowezesha kufikisha taarifa na huduma kwa jamii kwa urahisi na ufanisi zaidi kupitia vyombo vya habari.
Kwa upande wao, uongozi na wafanyakazi wa Uhondo Media walieleza kufurahishwa na ziara hiyo, wakisisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia kukuza mawasiliano bora, kubadilishana uzoefu, na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kujenga mahusiano ya kudumu kati ya taasisi za umma na vyombo vya habari.


