Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda anatarajiwa kuwasilisha ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenda kwa Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Dkt. Patrice Motsepe wa kuthibitisha dhamira ya Tanzania kuwa moja ya nchi mwenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Januari 16, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, saa chache kabla ya kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya ujumbe huo, Mhe. Makonda amesema
kuwa, hatua hiyo ni matokeo ya juhudi kubwa za Serikali katika kuimarisha sekta ya michezo hususan miundombinu ya viwanja, usafiri, malazi na maandalizi ya kiufundi yanayokidhi viwango vya kimataifa.
Ameongeza kuwa, Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 itakuwa ni fursa adhimu ya kutangaza sekta ya utalii, kuimarisha diplomasia ya michezo, pamoja na kukuza uchumi kupitia ajira na biashara zitakazotokana na mashindano hayo.


