Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa Jengo jipya la kisasa la Ofisi za Wizara ya Fedha, lililopo katika Mji wa Serikali-Mtumba, mkoani Dodoma, litawawezesha watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi katika mazingira bora na kuwahudumia wananchi pamoja na wadau wengine kwa ufanisi zaidi.
Jengo hilo la Wizara ya Fedha linajengwa na Mkandarasi Mkuu, Estim Construction Co. Ltd, huku Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) likishirikiana na IPA Architects Ltd katika usanifu na usimamizi wa ujenzi.

Mhe. Balozi Omar aliyasema hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa jengo hilo, akiwa ameambatana na Naibu Mawaziri wake wawili, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) na Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), pamoja na menejimenti ya Wizara ikiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Natu El-maamry Mwamba.
Katika ziara hiyo, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha ujenzi wa jengo hilo na kuhakikisha miradi ya kimkakati ya Serikali inatekelezwa kwa wakati. Aidha, aliwataka watumishi wa Wizara ya Fedha kulitunza jengo hilo na kusimamia ipasavyo mifumo yake ya ulinzi na usalama ili kudumisha thamani na matumizi yake ya muda mrefu.
Kwa upande wao, Naibu Mawaziri, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) na Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), walisema kuwa jengo hilo ni la kisasa na limejengwa kwa viwango vya juu, likiongeza hadhi ya Wizara ya Fedha na kuendana na dira ya Serikali ya ujenzi wa majengo bora ya ofisi.
Akitoa taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Msimamizi wa ujenzi wa jengo hilo, Mhandisi Japhet Mkwamira, alisema kuwa jenzi la ghorofa 11, ambalo ni jengo refu zaidi miongoni mwa majengo yote ya Serikali yaliyopo Mji wa Serikali-Mtumba kwa sasa, limekamilika kwa asilimia 98, na linatarajiwa kuanza kutumika mara baada ya hatua za mwisho kukamilika.


