WAKULIMA WAIPONGEZA NFRA KWA KUTATUA CHANGAMOTO KWENYE VITUO
Wakulima wanaouza mahindi kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika Mkoa wa Songwe wameishukuru na kuipongeza Serikali kwa kununua mazao yao kwa bei nzuri na kutatatua changamoto ya uhaba wa mifuko ya kufungashia mahindi katika vituo vya kununulia mahindi.
Wakulima hao wamezungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vituo vya Ofisi ya NFRA Songwe wilaya ya Mbozi, Soko la Kimataifa Tunduma wilaya Momba na kituo cha Kakozi wilayani Momba tarehe 1 Septemba 2024 ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Hussein Mohammed Omar aliongoza mikutano hiyo na kuweza kuwasikiliza wakulima.
Akitoa shukrani zake kwa Serikali, mkulima Frank Masiani amemueleza Dkt. Omar kuwa viongozi wa NFRA wamefanya juhudi kubwa za kuhakikisha wanapata mifuko ya kufungashia na kupelekea mzigo uliyofungashwa kuwa mkubwa na kuiomba Serikali isadie kuongeza nguvu kazi ili mahindi yaliyofungashwa yaondolewe kwa wakati.
Aidha, Bw. Masiani amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwasaidia kupata soko na kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa zoezi la ununuzi. “Kazi iliyofanya kubwa sana, tumeteseka hapo nyuma sasa tumepata mifuko kwa wakati mzigo uliofungashwa umekamilika sasa tunaomba kasi ya uondoaji wa mzigo iongezwe,” amesema Bw. Masiani.
Kwa upande wake, Bw. Medius Kibonde anayeuza mahindi yake kwenye kituo cha Kakozi wilayani Momba amesema kwa sasa kasi ya kuuza na kununu mahindi imeongezeka na hakuna mkulima anayekaa muda mrefu kituoni hapo.
Akijibu hoja zilizowasilishwa na wakulima kwenye vituo vya mauzo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Hussein Mohamed Omar amewapongeza wakulima hao kwa kazi nzuri na kuwaeleza kuwa ongezeko la uzalisha wa mahindi ni matokeo ya juhudi za Serikali za kuwawezesha wakulima kupata mbolea kwa bei ya ruzuku.
Dkt. Omar ameelekeza uongozi wa NFRA wakutane na msambazaji wa mifuko na wakubaliane juu ya uwezo wake wa kusambaza kiasi kitakachokidhi mahitaji na endapo uwezo wake utakuwa mdogo kuliko mahitaji basi watafute msambazaji mwingine ili wakulima wasisumbuke tena.