TRA KUKUTANA NA WADAU WA SEKTA YA MADINI KUJADILIANA MABORESHO YA SEKTA YA MADINI
Dar es salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) inajiandaa kufanya mkutano mkubwa na wadau wa sekta ya madini ili kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kuiimarisha sekta ya madini na pia kuiongezea nchi mapato kupitia sekta hii.
Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es salaam kufuatia kikao cha pamoja kati ya Wizara ya Fedha na Wizara ya Madini kujadili namba bora ya ushirikiano baina ya Wizara hizi ili kukuza sekta ya madini kwenye kikao kilichoongozwa na Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde.
“Sekta ya Madini ni sekta ambayo ina nafasi kubwa katika kuchangia mapato ya nchi yetu ya Tanzania.
Makusanyo ya mapato kupitia sekta ya madini yanaendelea kukua na kuongezeka kila mwaka mpaka kufikia Tsh 753bn kwa mwaka 2023/24 na mwaka huu tumejipanga kukusanya Shilingi Trilioni moja.
Zipo changamoto kadhaa za kikodi ambazo TRA wakikaa na wadau na kuzijadili kwa pamoja kutafuta suluhisho,sekta hii itapaa na kuwa mojawapo ya sekta kiongozi za kukuza uchumi wetu”Alisema Mavunde
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Ndg. Elijah Mwandumbya ameeleza umuhimu wa majadiliano na sekta ya madini kwa kuwa ni sekta ambayo mchango wake kwenye uchumi wa Tanzania unaonekana na hivyo kuelekeza TRA kukutana na wadau wake kwa haraka ili kupata ufumbuzi wa pamoja wa baadhi ya masuala ya kikodi yanayoleta changamoto.
Akitoa maelezo kwenye mkutano huo,Kamishna Mkuu wa TRA *Ndg. Yusuph Mwenda * ameipongeza sekta ya madini kwa mchango wake mkubwa kwenye makusanyo ya kodi na kukuza uchumi wa Tanzania na kuahidi kuitisha kikao cha haraka ili kuzungumza na wadau juu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya madini ili kusaidia kuchochea ukuaji na mchango wa sekta katika uchumi wa Tanzania.