NHC MSISAHAU MALENGO YENU KWA WATANZANIA – NDEJEMBI

0

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuendelea kutekeleza malengo yake ya msingi kwa kuwajengea watanzania wa kipato cha chini makazi bora na yenye gharama nafuu.

Mhe Ndejembi ameyasema hayo leo Agosti 07, 2024 wakati akizungumza na Menejimenti na Watumishi wa NHC kwenye ziara yake ya kujitambulisha kwa watumishi wa shirika hilo baada ya kuteuliwa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Julai 21, 2024.

“Tusisahau kuwajengea watanzania maskini makazi bora na yenye gharama nafuu. Tuweke mipango madhubuti kuhakikisha tunatimiza azma hii. Shirika lazima liendelee na miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi hususani wale wa kipato cha chini.’

“ Ni lazima tuhakikishe hakuna wizi wala ubadhirifu wa fedha za umma hasa katika ununuzi wa ardhi. Ni muhimu kuzingatia uhalisia wa ardhi tunayoinunua,” amesema Mhe. Ndejembi.

Aidha, Mhe. Ndejembi amelipongeza Shirika hilo kwa kuanzisha mpango wa Samia Housing Scheme ambao unalenga kujenga nyumba 5,000 ambapo awamu ya kwanza limeanza kujenga nyumba hizo katika jiji la Dar es Salaam na nyumba 560 nyingine zinatarajiwa kujengwa Dodoma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah amemhakikishia Mhe. Waziri Ndejembi kwamba shirika hilo litaendelea kutekeleza malengo yake ya msingi ya kujenga nyumba zenye ubora na gharama nafuu kwa kuzingatia kipato cha kila mtanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *