MBUNGE MAVUNDE AWAPONGEZA WALIMU DODOMA KWA MIKAKATI YA KUJIINUA UCHUMI

0

Mbunge wa Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde amewapongeza walimu wanawake wa Dodoma kwa mikakati ya kujiinua kiuchumi na kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo mkoani Dodoma.

Mavunde ameyasema hayo wakati akizindua SACCOS ya Walimu Mkoa wa Dodoma ambayo inaundwa na walimu wa wilaya mbalimbali za Mkoa wa Dodoma ambayo ina lengo kuu la kusaidia upatikanaji wa mitaji kwa walimu hao wambao wanashiriki shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Najua jukumu lenu la kwanza ni kufundisha,lakini pia sio dhambi ninyi kushiriki katika shughuli za kiuchumi ila mradi tu iwe nje ya muda wako wa kazi na pia kama haiathiri majukumu yako ya msingi ya ufundishaji.

Nimefurahi sana leo kuona mmeanzisha hii SACCOS maalum kwa ajili ya walimu kama njia ya uwezeshwaji kiuchumi kwa walimu.

Nategemea kupitia SACCOS hii itasaidia kupatikana kwa mitaji ambayo itakuwa chachu ya uanzishwaji wa miradi ya kiuchumi na hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa Dodoma kuna fursa nyingi za kiuchumi na hivyo ni muhimu kuzichangamkia mapema”Alisema Mavunde

Akizungumza katika Hafla hiyo,Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Mh. Fatma Toufiq amepongeza jitihada za walimu wakinamama za kujiletea maendeleo na kuwataka kuchangamkia fursa mbalimbali za maendeleo na kuahidi kuwaunga mkono katika shughuli za maendeleo.”

Katika hafla hiyo,Wabunge Mavunde na Toufiq wamechangia Tsh 10,000,000 kuiendeleza SACCOS hiyo ya walimu.

Naye muandaaji wa Kongamano la Walimu Wanawake Mkoani Dodoma,Mwl. Sheila Chinja amesema lengo kuu la kuwakutanisha walimu wanawake ni kujadili kwa pamoja na kuwaendeleza kiuchumi na ndio maana likaja wazo la uanzishwaji wa SACCOS hii maalum kwa lengo la kuwawezesha walimu.

Mwl. Sheila pia amemshukuru Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kwa kuboresha mazingira mazuri ya ufundishaji kwa kuboresha miundombinu ya Elimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *