WATAALAMU WAASWA KUPELEKA TEKNOLOJIA YA MIFUGO NA UVUVI VIJIJINI
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amewaasa wataalamu wa sekta za mifugo na uvuvi kupeleka na kufundisha teknolojia za sekta hizo vijijini ili kuwapa wafugaji elimu ya kutosha kuhusu ufugaji wa kisasa kwa lengo la kuleta tija.
Akizungumza, leo Agosti 4, 2024 Mkoani Dodoma alipotembelea kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa (Nane Nane) 2024 yanayofanyika Kitaifa mkoani humo, Mhe. Senyamule amesema wataalamu wahakikishe teknolojia za kisasa zinawafikia wadau wote wa mifugo na uvuvi, hususan maeneo ya vijijini.
“Wataalamu wachukue hatua ya kwenda kwenye makundi ya wafugaji ili kwenda kuwaelimisha kuhusu teknolojia mpya ya ufugaji na kuhakikisha inawafikia” amesema Mhe. Senyamule
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mheshimiwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya mapinduzi makubwa sana katika sekta za mifugo na uvuvi kwani ameshuhudia teknolojia mbalimbali na nzuri katika mabanda ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mhe. Senyamule alisema sekta binafsi pia zimepokea mabadiliko hayo ya kiteknolojia, hususan upande wa vijana wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ambao wanatumia teknolojia hizi kama ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Pia, ametoa wito kwa wadau wote wa mifugo na uvuvi kutumia fursa hii ya maonesho haya ya Nane Nane ili kuweza kujifunza na kupata ufahamu juu ya teknolojia za kisasa za mifugo na uvuvi