MRADI WA TAZA KUUNGANISHA UMEME AFRIKA
Serikali imesema kuwa mradi mkubwa wa usafirishaji umeme wa TAZA unaohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga na kuunganisha Tanzania na Zambia (TAZA) pamoja na vituo vya kupoza umeme vya Tagamenda, Kisada, Iganjo, Nkengamo na Malangali utawezesha kuunganisha Bara la Afrika kwa nishati ya umeme kutoka Afrika Kusini hadi Ethiopia.
Hayo yameelezwa leo Julai 29, 2024 Sumbawanga mkoani Rukwa na
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akiweka jiwe la msingi la utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa usafirishaji umeme ambao unahusisha
kipande cha kilomita 4 kutoka Tunduma hadi Nakonde mpakani mwa Tanzania na Zambia.
“ Kwa kutambua kuwa nishati ni kichocheo cha uchumi, Serikali imeendelea kutekekeza miradi mbalimbali ukiwemo wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao tayari unaingiza megawati 705 kwenye gridi ya Taifa na hivyo kuwezesha nchi kuwa na ziada ya umeme huku mtambo mwingine wa megawati 235 ukitarajiwa kuwashwa mwezi Agosti”, amesema Dkt. Biteko.
Ametaja miradi mingine inayotekelezwa kuwa ni wa umeme Jua wa Kishapu (MW 150), Malagarasi (MW 49.5) na ya Gesi Asilia huku lengo likiwa ni kuwa na uhakika wa umeme wa kutosha.
Pamoja na utekelezaji wa miradi hiyo, Dkt. Biteko amesema uzalishaji wa umeme lazima uende pamoja na kazi ya uungashiaji umeme wananchi kupitia miradi mbalimbali kama wa TAZA ambao unawahakikishia Wanarukwa upatikanaji wa umeme wa gridi ambao utakuwa wa uhakika na wa kutosha.
Amesema kwa sasa Mkoa wa Rukwa unapata umeme kwa kiasi kikubwa kutoka nchini Zambia kwa gharama ya shilingi bilioni 15 kwa mwaka hivyo kukamilika kwa mradi huo kutaifanya Tanzania kuacha kununua umeme kutoka nchi hiyo isipokuwa nyakati za dharura.
Ameongeza kuwa, mradi wa TAZA utafaidisha pia maeneo yanayopitiwa na mkuza kutoka mkoani Iringa hadi Rukwa kupitia vituo vya kupoza na kusambaza umeme na kuwezesha kufanyika kwa biashara ya umeme katika nchi zilizopo Mashariki mwa Afrika kupitia Southern African Power Pool (SAPP) na Easten Africa Power Pool (EAPP).
Kuhusu usimamizi wa mradi huo, Dkt, Biteko pamoja na kuipongeza TANESCO kwa utendaji mzuri wa kazi, ameiagiza taasisi hiyo kuhakikisha kuwa kasi ya utekelezaji mradi wa TAZA inaendelea kuwa kubwa, na kwamba tukio la kuwekwa kwa jiwe la msingi lisiishie kwenye kupiga picha na kisha kutokomea bali wausimamie mradi huo ili ulete matokeo tarajiwa.
Akigusia usambazaji wa umeme vijijini mkoani Rukwa, Dkt.Biteko amesema kuwa Serikali haifurahishwi na kasi yake ya utekelezaji wa miradi kwani analalamikiwa kusuasua na hivyo ameagiza kuwa ifikapo Agosti mwaka huu awe amemaliza kazi na asipotekeleza agizo hilo achukuliwe hatua za kimkataba na hii inajumusha pia wakandarasi wengine wazembe ikiwemo katika Mkoa wa Kagera.
“Kazi za umeme vijijini zinaombwa na kampuni za nje ya nchi na kampuni za ndani, tunaonekana wabaya kwa kuzibana sana kampuni za nje lakini za ndani tunabembelezana, Katibu Mkuu na DG REA nataka nione hatua zinachukuliwa, haiwezekani wakandarasi wageni tunawabana halafu wa ndani wanaharibu miradit, wananchi wanalalamika halafu tunabembelezana, hii hapana.” Amesisitiza Dkt. Biteko
Amesema Serikali inataka kumaliza kazi ya usambazaji umeme vijijini na kuhamia vitongojini na kwamba lengo ni kuwa ifikapo mwezi wa 12 mwaka huu vijiji vyote viwe vimesambaziwa umeme.
Kuhusu utekelezaji wa TAZA, Dkt. Biteko ameshukuru Wafadhili wa mradi huo ambao ni Benki ya Dunia (WB), Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) ambao kwa pamoja wametoa zaidi ya shilingi Trilioni Moja za kutekeleza mradi huo ambao pia unahusisha ujenzi wa vituo vitano vya kupiza umeme. Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inawajali wafadhili wetu.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali itaendelea kuipa kipaumbele ajenda husika kwani imeshaanzisha Kitengo cha kushughulikia nishati hiyo ndani ya Wizara na kwamba Benki ya Dunia imeahidi kuangalia namna ya kuiwezesha Serikali kutekeleza ajenda hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere amesema mradi wa TAZA utaihakikishia Rukwa umeme wa uhakika, pia kuimarisha uwekezaji ambapo amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini ambapo tayari vijiji 308 vina umeme huku 31 vilivyobaki kazi ikiendelea.
Kwa upande wake, Katibu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema mradi wa TAZA ni wa kipekee kwa sababu utawezesha Afrika kuunganishwa na umeme kutoka Afrika Kusini hadi Ethiopia.
Naye, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Mathew Mkingule ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa umeme wa TAZA ambao amesema utahakikisha usalama wa nishati katika nchi za Kusini mwa Afrika, kukuza uchumi Mkoa wa Rukwa, kuwezesha biashara ya umeme, fursa ya ajira na kulinda mazingira kwani nishati ya umeme inawezesha wananchi kutumia nishati hiyo katika kupikia.
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete kwa niaba ya Wawekezaji wa mradi amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko pamoja na Serikali kwa ujumla kwa miongozo ambayo imewezesha mradi wa TAZA kuanza kutekelezwa.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alieleza kuwa, mradi wa TAZA ni sehemu ya maazimio ya yaliyofanyika tarehe 15 Desemba 2014 baina ya Tanzania, Kenya na Zambia ya kuunganisha gridi za nchi hizo tatu.
Katika utekelezaji wa makubaliano hayo, amesema Tanzania ilianza kujenga laini ya umeme ya kV 400 ya km 670 kutoka Dodoma hadi Shinyanga ambayo ilishakamilika na baadaye kujenga laini ya kV 400 kutoka Singida hadi Namanga kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya ambao umekamilika kwa asilimia 99.8 na kipande cha tatu ni cha mradi wa TAZA ambacho kinatekelezwa sasa ili kuunganisha gridi ya Tanzania na Zambia.
Amesema mradi umeshaanza na umefikia asilimia 29.8 huku ukitarajiwa kukamilika Mei 2026.
Wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ni Naibu Katibu MKuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa kamati mbalimbali za Bunge ikiwemo ya Bajeti, Hesabu za Serikali, Nishati na Madini, Mwakilishi wa AU, na AFD, Katibu Mtendaji wa EAPP, Bodi na Wakurugenzi wa Taasisi chini ya Wizara, Menejimenti Wizara ya Nishati pamoja na Watendaji kutoka Shirika la Umeme la Zambia (ZESCO).