WAZIRI MAVUNDE AWABAINI WATUMISHI WASIO WAAMINIFU NDANI YA SEKTA YA MADINI

0

Waziri wa Madini Mhe. Antony Mavunde ametoa Onyo kwa watumishi wa Sekta ya Madini wanaoitumia sekta hiyo kujinufaisha kwa maslahi yao Binafsi

Ametoa Onyo hilo leo Julai 28, 2024 wakati Akitoa Taarifa kwa Vyombo vya Habari Ofisini kwake Jijini Dodoma.
Waziri Mavunde amesema licha ya mafanikio makubwa katika Wizara hiyo bado kuna watumishi wasio waaminifu waliopo wanaosababisha Serikali kupoteza mapato na kwamba Operesheni Maalum inaendelea kufanyika na atapeleka majina yao kwa Katibu Mkuu ili waweze kuchukuliwa Hatua mara moja

“Katibu Mkuu tukikuletea majina chukua hatua kwa haraka, kuna baadhi ya watu wanaitumia sekta hii kwaajili ya mifuko yao binafsi, sisi tumeweka malengo makubwa ya kukusanya fedha ili kuisaidia Serikali yetu na kuisaidia nchi yetu lakini wako wachache ambao wana mitizamo tofauti” Amesema Waziri Mavunde

Aidha, Waziri Mavunde amekemea vitendo vya udanyanyifu kwenye biashara ya madini pamoja na utoroshaji wa madini vinavyofanywa na watu wachache ambao katika vitendo vyao, ambao wanarudisha nyuma malengo na kusema Wizara itaendelea kuchukua hatua kali kwa wahusika wote watakaobainika wanajihusisha na utoroshaji wa madini.

Pia amepiga marufuku, tabia ya wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini kuingia makubaliano yasiyo rasmi na wageni kutoka nje ya nchi na kuwaruhusu kufanya kazi katika leseni zao.

“Ikumbukwe kwamba, leseni za uchimbaji mdogo wa madini zinatolewa kwa Watanzania pekee kwa mujibu wa Kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Madini, Sura 123. , Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Madini, Sura 123 kimeweka wazi kwamba, kwa mmiliki wa leseni ndogo ya uchimbaji wa madini, pale atakapohitaji msaada wa kiufundi ambao haupatikani nchini, anaruhusiwa kuingia makubaliano na mgeni kutoka nje ya nchi kupata huduma hiyo baada ya makubaliano hayo kupitishwa na Tume ya Madini.”

Hata hivyo, Athari kubwa zinazotokana na kutozingatiwa kwa kifungu cha 8(3) ni pamoja na; wachimbaji wengi wadogo waliokuwa wakiendelea na shughuli zao za uchimbaji katika leseni husika huathirika kwa kukosa ajira, kupoteza mitaji yao waliyowekeza wakati wa uchimbaji pia huleta chuki kwa Serikali yao.

“Nachukua nafasi hii kupiga marufuku kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini, kuingiza wageni kutoka nje ya nchi kwenye leseni zao bila kuwa na mikataba/makubaliano ya msaada wa kiufundi (Technical Support) yaliyopitishwa kwa mujibu wa Sheria., Pia nichukue fursa hii kupiga marufuku wageni wenye leseni kubwa za biashara ya madini (dealer’s Licence) hususan wa madini ya vito kwenda machimboni kukusanya madini. Kufanya hivi ni kupora haki ya ajira ya Watanzania ambao kwa mujibu wa Sheria,kazi ya kufuata madini machimboni inapaswa kufanywa na Watanzania pekee wenye kumiliki leseni ya “broker”. ” amesisitiza Waziri huyo

Waziri Mavunde pia amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini pamoja na wageni kutoka nje ya nchi watakaobainika kukiuka matakwa ya Sheria.

Katika hatua nyingine ametoa Taarifa kuwa ndani ya kipindi kifupi kumeshuhudiwa ongezeko la makusanyo ya maduhuli yatokanayo na shughuli za uchimbaji wa madini ambapo Hapo nyuma kidogo, Wizara ilikuwa ikikusanya kiasi kidogo cha maduhuli ukilinganisha na sasa. Mathalan, Mwaka wa Fedha 2014/2015, Wizara ilikuwa na lengo la kukusanya Shilingi 209,957,882,999.00 na kufanikiwa kukusanya TZS 168,043,402,877.13. Aidha, Mwaka wa Fedha 2015/2016 lengo la makusanyo lilikuwa ni Shilingi 211,957,882,999.00 na kufanikiwa kukusanya Shilingi 207,917,127,854.55.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *