DKT. TULIA AISHUKURU SERIKALI YA RAIS SAMIA KUTATUA KILIO CHA WANANCHI MBEYA

0

Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha Wananchi wa Mbeya kwa hatua ya kuanza kuboresha miundombinu mbalimbali katika Jiji la Mbeya ikiwemo barabara ambazo zimekuwa kero kwa miaka mingi.

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 27 Julai, 2024 wakati wa hafla ya utiaji saini Mikataba ya miradi ya TACTIC ujenzi wa barabara, Kituo Kikuu cha Mabasi na Soko Kuu la Jiji hilo iliyofanyika katika Viwanja vya Aiport ya zamani ambapo Mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa.

Ameleza kuwa, pamoja na Jiji hilo kuwa na changamoto nyingi suala la barabara limekuwa kikwazo zaidi kutokana na maeneo mengi kutopitika ikiwemo barabara za mitaa hivyo kurudisha nyuma shughuli za maendeleo kwa Wananchi.

Sambamba na hayo, Dkt. Tulia amebainisha kuwa baada ya kutoa kilio hicho cha Wananchi tayari Serikali imekwishaanza kufanyia kazi maeneo mbalimbali kwa kujenga barabara za mitaa kwa kiwango cha lami ikiwemo barabara kuu ya njia nne Igawa-Ifisi.

Kwa upande wake Waziri Mchengerwa amesema kuwa Wizara yake imepokea maelekezo mahususi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha inatekeleza maombi yote yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Dkt. Tulia ya kuhakikisha inazitatua changamoto zote zikiwemo za barabara, elimu, afya n.k

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *