WANANCHI WA VUNJO WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO ILI KUFANIKISHA UJENZI WA MASOKO YA KISASA

0

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amewataka wananchi wa jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro kutoa ushirikiano kwa wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo watakaoenda jimboni humo kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa masoko ya kisasa ya mazao ya kilimo.

Mhe. Silinde amesema hayo tarehe 24 Julai, 2024 alipofanya ziara katika masoko ya mazao ya kilimo ya Lyamwombi, Kisambo, Mwika na Himo yaliyopo katika jimbo la Vunjo, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

“Mwaka huu tutafanya usanifu wa kina kwa ajili ya kupata gharama halisi za ujenzi wa ili masoko ya Lyamwombi, Kisambo, Mwika na Himo yaingizwe kwenye mipango ya ujenzi katika mwaka ujao wa fedha; nawasihi sana watakapofika wataalamu wa Serikali wapeni ushirikiano ili mipango hii itekelezwe kwa wakati,” amesema Mhe. Silinde.

Mhe. Silinde amesema Wizara ya Kilimo itajenga masoko hayo katika ubora unaohitajika ikiwa ni pamoja na miundombinu ya kuhifadhia mazao ya wakulima ili yafike kwa walaji yakiwa na ubora na hatimaye wakulima na wafanyabiashara waondokane na hasara zinazosababishwa na kuharibika kwa mazao baada ya kuvunwa.

Mhe. Silinde amesema Serikali imejiridhisha kuwa itakapokamilisha miradi ya masoko hayo wananchi wataweza kunufaika kibiashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Mhe. Dkt. Charles Kimei ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utayari wa kuboresha masoko hayo amboyo ni muhimu kwa uchumi wa wakulima wa jimbo hilo na Taifa kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *