IJUE DHANA YA VISION 2030: MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI

0

Kwanini Madini ni Maisha?

Vision 2030 inabebwa na dhana nzima ya umuhimu wa madini katika maisha ya kila siku ambapo uwepo wa madini na miamba ya madini unagusa maisha ya kila mtu. Kuwepo kwa madini, kunawezesha watu kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na hivyo kujiingizia vipato vya moja kwa moja na vipato vingine vinavyotokana na shughuli za biashara kama za chakula ikiwemo za utoaji huduma, usambazaji wa vifaa vinavyohitajika kwenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini.

Kwa kuzingatia hayo, Sera ya Madini ya mwaka 2009 imesisitiza juu ya kufungamanisha madini na sekta nyingine hivyo, Vision 2030 inalenga kuboresha maisha ya watu kupitia sekta mbalimbali.

Kama inavyofahamika duniani kote, uchimbaji wa madini huwa na tija endapo ukiendeshwa kisayansi, hii inapunguza upotevu wa mitaji na uhifadhi wa mazingira kwa kufuata maeneo yenye rasilimali madini pekee. Kwa Tanzania, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ndiyo mzalishaji wa taarifa za awali za jiosayansi ambazo zinatoa mwongozo wa mahali yalipo madini na aina yake katika sehemu mbalimbali nchini. Jambo hili ni muhimu sana kwa wachimbaji wadogo na wakubwa Tanzania kama ilivyo kwenye nchi nyingine zenye shughuli za uchimbaji wa madini zilizoendelea.

Kwa Tanzania, GST ndiyo inajua jiolojia ya nchi na ni muhimu sana kutumia taarifa zao ili kupata mwongozo katika kuendesha shughuli za uchimbaji. Kwa mfano, migodi mingi iliyoanzishwa nchini ikiwemo ile ya Geita Gold Mining Limited (GGML) na Bulyanhulu ilianzishwa kutokana na taarifa za tafiti za miaka ya nyuma za GST. Pamoja na hiyo, hata migodi inayotarajiwa kuanza kama ile ya Kabanga Nickel ni kazi zilizofanywa na GST kipindi cha nyuma mnamo mwaka 1978.

Hivyo, ili kuwepo na manufaa zaidi ya Sekta ya Madini kwenye uchumi na maendeleo ya nchi ikiwemo kuchangia zaidi ya asilimia 10 ya mchango wa Sekta ya Madini katika pato la taifa, Serikali inakusudia kuiwezesha GST kuzalisha taarifa za kina kupitia tafiti za jiofizikia (High Resolution) kupitia Vision 2030 ambazo zitavutia uwekezaji kwa Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), wachimbaji wakubwa na wadogo. Kwa sasa tafiti za kina za jiofizikia zinahitajika ili kurusha ndege kwa ajili ya kupata taswira halisi ya miamba inayobeba madini chini ya ardhi ilipo katika sehemu mbalimbali za nchini.  Jambo hili (High resolution) mpaka sasa limefanyika kwa asilimia 16 tu na bado maeneo mengi yanahitaji kuibuliwa fursa zake kwa ajili ya kuvutia uwekezaji kwa watanzania na wageni kutoka nje ya nchi.

Sekta ya Kilimo na Maji

Kama inavyofahamika mwanadamu anahitaji chakula ili aweze kuishi. Chakula anachokula kinapatikana kwa kulima. Kilimo kinahitaji mbolea ili kuweza kukuza mazao katika ubora unaohitajika na mbolea hizo zinatokana na madini mbalimbali. Kadhalika, dunia inahitaji kuongeza uzalishaji wa mazao na kuwa na hifadhi ya chakula cha kutosha, hivyo, uzalishaji wa chakula cha kutosha unahitaji mbolea. Chukua mfano Tanzania inaagiza mbolea kwa kiasi cha asilimia 90 kutoka nje. Ili kupunguza hali hiyo ya kuagiza mbolea ni muhimu kuzalisha mbolea hapa hapa nchini. Mbolea kama UREA inahitaji gesi kutoka kwenye makaa ya mawe, DAP inahitaji Madini ya Phosphorus, NPK inahitaji Nitrogen, Phosporus na Potassium na n.k.  Mbolea hizi zinatokana na madini ambayo GST kulingana na jiolojia ya nchi, kupitia Vision 2030, GST itaweza kutafuta na kuainisha maeneo hayo ambayo yatakuwa vyanzo vya madini husika.

Kwa taarifa zilizopo, hivi sasa nchi ya Tanzania ina takribani hekta milioni 3.7 zinazohitaji chokaa kwa ajili ya kilimo na hekta milioni 3.6 zinahitaji madini ya jasi kwa ajili ya kurekebisha tindikali na chumvi zilizoko kwenye udongo.  Hivyo, uwepo wa madini ya chokaa na jasi ni fursa ya kuanzisha viwanda vya kuchakata chokaa na jasi nchini kutokana na upatikanaji wa malighafi hizo.

Pia, GST katika shughuli ya jiosayansi kupitia jiofizikia itabainisha mikondo ya maji iliyopo chini ya ardhi kwenye miamba inayohifadhi maji. Hii itasaidia katika kufanya mipango ya maendeleo kwa wananchi ikiwemo kilimo cha umwagiliaji kwa uzalishaji wa uhakika wa chakula na matumizi mengine ya maji kwa jamii na mifugo.

Kitaalam kuna miamba inayobeba maji ijulikanayo kama aquifer, ambapo ndipo yanapopatikana maji safi kutoka kwenye ardhi na maji hayo kutumika kwa matumizi ya nyumbani. Kupitia vision 2030, utafiti utafanyika wa high resolution geophysical survey ambao utawezesha kubaini miamba hiyo. Hii itasaidia Serikali kuwezesha wananchi kupata maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na hivyo kufanikiwa katika usemi usemao “maji ni uhai” yaani ni “maisha”. Sambamba na kupata maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kuna uwezekano kwa kushirikiana na Sekta kilimo kuwezesha wananchi kuanzisha scheme kubwa za umwagiliaji kutokana na visima vitakavyochimbwa kwenye miamba itakayokuwa imebeba maji.  Hivyo, kilimo cha uhakika kitapatikana kutokana na shughuli za kilimo na kwa kufanya hivyo kutaboresha maisha ya watu. Hii ndiyo maana ya dhana ya madini ni “Maisha”

Kwa lugha nyepesi ni kwamba kupitia vision 2030 itafungamanisha madini na kilimo kupitia taarifa za utafiti wa kijiolojia kwa kuainisha aina ya udongo kulingana na jiolojia ya eneo husika. ‘’Badala ya Serikali kuagiza mbolea nje ya nchi taifa litaweza kuzalisha mbolea hapa hapa nchini. Hivi  sasa, Tanzania inaagiza nje ya nchi tani takribani 350,000 za mbolea kwa kutumia fedha za kigeni kwa ajili ya mbolea ya kupandia, kukuzia na kustawisha,’’ anasema Waziri Mavunde katika moja ya mikutano yake wakati akielezea umuhimu wa vision 2030 katika sekta ya kilimo.

Sekta ya Nishati na Uhitaji wa Madini Muhimu

Baadhi ya maeneo ya nchi yetu yapo katika bonde la ufa ambapo kuna uwezekano  mkubwa wa vyanzo vya jotoardhi (Geothermal). Hiki ni chanzo mojawapo cha nishati safi ambalo ndio kusudio la dunia la kuzalishwa kwa nishati kutoka katika vyanzo visivyotoa hewa ya ukaa ambayo ni hatari kwa maisha na mazingira. GST kupitia tafiti zake kwenye bonde la ufa imebainisha maeneo kadhaa yenye uwepo wa joto ardhi na inaweza kuendelea kuibua vyanzo muhimu vya joto ardhi ambayo itasaidia katika kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme kwenye vyanzo vya sasa vilivyopo.

Aidha, mwelekeo wa dunia sasa ni matumizi ya madini muhimu na mkakati katika uzalishaji wa vifaa vya teknolojia kama vile  betri za magari ya umeme, vifaa vya umeme wa solar na upepo n.k. Madini haya hayakuwa yanazalishwa kwa uhitaji mkubwa hapa nchini. Hivyo, kupitia mkakati wa vision 2030, utafiti wa kina utabainisha madini hayo katika maeneo mbalimbali ya nchi na hatimaye kuvutia uwekezaji mkubwa kwenye mnyororo wote wa madini hayo. Kwa kufanya hivyo Tanzania inajiweka kwenye sura ya dunia kama mdau muhimu kwenye eneo hili la nishati safi dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi duniani. Madini hayo ni kama nikeli, kolbati, lithium, kinywe na manganese na mengine mengi.

Kwanini Madini ni Utajiri?

Ieleweke kuwa, Vision 2030 inamaanisha ifikapo mwaka 2030, ni matarajio ya Wizara ya Madini kuwa nchi ya Tanzania iwe imefanyiwa utafiti wa kina kwa njia Geophysical Airborne Survey kwa walau asilimia 50. Kimsingi, taarifa za utafiti ndizo zinazoshawishi uwepo wa uwekezaji na hivyo kwa kufanya hivyo itawezesha kupata uwekezaji wa uhakika. Hivyo, taarifa za uwepo madini ni utajiri kwa kuwa kutawezesha ushiriki wa wawekezaji kwa uhakika ikiwemo wachimbaji wadogo ambao wamekuwa ni wahanga wa kuchimba kwenye maeneo yasiyokuwa na taarifa na hivyo wengi wao wameishia kupoteza fedha zao na kupoteza matumaini kuwekeza kwenye madini.

Aidha, mapato yanayopatikana  sasa yanatokana na taarifa chache za uwepo wa madini, hivyo, kuongezeka kwa uhakika wa taarifa kutawezesha washiriki wengi na hivyo kuifanya nchi pamoja na wananchi kupata fedha nyingi na kwa kufanya hivyo inaashirikia kuwa MADINI NI UTAJIRI

Sekta ya Ujenzi

VISION 2030 imelenga kuchochea ukuaji wa Sekta ya viwanda vya uchakataji madini nchini kwa kutumia malighafi mbalimbali za madini zitakazo patikana kutokana na taarifa za utafiti wa kina na hivyo kuwa chanzo cha kuimarisha uchumi wa taifa kupitia mapato yatokanayo na rasilimali madini. Uanzishwaji wa viwanda ambavyo vinatumia malighafi madini ni muhimu sana katika nchi yetu ili kuzalisha bidhaa kama vile saluji, jasi, marumaru, na nakshi mbali mbali zinazoagizwa kutoka nje ya nchi na kiasi fulani zinazalishwa hapa nchini. Jiolojia ya nchi yetu inayo madini ya aina nyingi sana yakiwemo ya viwandani yanayopatikana katika maeneo ya ukanda wa pwani kama vile kisarawe, Tanga, na Mtwara.

Aidha, Madini ya vito yanatumika kutengeneza marembo ya bidhaa za usonara. Kwa ufupi, Sekta ya madini inatoa fursa za ajira kupitia shughuli za utafutaji wa madini, uchimbaji, uchakataji wa madini na uzalishaji wa bidhaa.  Endapo kutakuwa na ustawi wa shughuli za utafiti utawezesha kutoa ajira nyingi, kuongeza mapato ya Serikali na hivyo kuendeleza uchumi wa nchi. Haya yote yanafanya Madini kuwa maisha na utajiri.

Sekta ya Utalii na makumbusho

Kupitia Vision 2030, GST kwa kushirikiana sekta ya utalii wanaweza kuibua vyanzo vipya vya utalii nchini unaojulikana kama utalii wa kijiolojia kwa maana ya geotourism. Yapo maeneo muhimu yana jiolojia ya aina ya pekee sana duniani ambayo yanaingiza fedha nyingi katika nchi nyingine kama China.

Chunguzi za Maabara za jiosayansi

Serikali inaendelea kuboresha GST pamoja na huduma zake za maabara ambayo ndiyo maabara pekee ya Serikali ya jiosayansi hapa nchini inayofanya uchunguzi wa sampuli za miamba, udongo, maji, makinikia, na uimara wa miamba n.k.  Uimarishaji wa GST ni pamoja na ujenzi wa jengo la kisasa ambalo litatoa huduma bora zaidi ya sasa.

Kwa kifupi tu hii ndiyo dhana ya Vision 2030: Madini ni Maisha na utajiri. Yapo mengi kupitia dhana hii lakini kupitia makala hii imejaribu kueleza kwa kifupi tu.

#Vision 2030: Madini ni Maisha & Utajiri
#InvestInTanzaniaMiningSector

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *