TANESCO YAWEKA KAMBI MAGOMENI KOTA KUTOA ELIMU YA MABORESHO MFUMO LUKU

0

Na. Noel Rukanuga – DSM

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kinondoni Kusini limeendelea na zoezi la kuwaelimisha na kuhamasisha wateja wake kuhusu kufanya maboresho ya mfumo wa mita za Luku ambao umeaza kufanya maboresho kuanzia Julai 22, 2024 ikiwa na lengo la kuendana na mabadiliko ya mfumo wa mita za luku ya Kimataifa pamoja na kuongeza ufanisi na usalama.

Akizungumza leo Julai 23, 2024 wakati akitoa elimu  ya maboresho ya mfumo wa Luku kwa wateja wa Magomeni Kota,  Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini Mhandisi Florence Mwakasege,  amesema kuwa wanaendelea na zoezi la kuwaelimisha wateja katika maeneo mbalimbali katika Mkoa huo ili kuhakikisha wanafanya mabadiliko ya mfumo wa luku kwa wakati.

Mhandisi Mwakasege amesema kuwa lengo ni kuwasaidia wateja kuweza kufanya maboresho kwenye mita zao kwani tunataka wateja wetu wasipata shida wakati wananunua umeme na kuingiza  katika mita zao.

Amesema kuwa  mteja atakaponunua umeme kwa mara ya kwanza na atapokea tokeni zenye  tarakimu za makundi matatu ambapo kila kundi litakuwa na tarakimu 20.

Amesema kuwa kundi la kwanza na pili la tarakimu litakuwa kwa ajili ya maboresho ya mfumo wa luku, huku kundi la tatu kwa ajili ya umeme utakaokuwa umenunuliwa na mteja.

“Mteja ataingiza umeme tarakimu za kila kundi katika luku yake kwa mfatano unaosomeka kwenye risiti ya malipo au ujumbe mfupi wa maandishi (sms) na kila utakapoingiza kundi moja mteja anapaswa kubonyeza alama ya kukubali ya # au msale wa kukubali na hapo utakuwa umefanikiwa kuboresha mita yako na kupokea kiwango cha umeme ulionunua” amesema Mhandisi Mwakasege.

Mhandisi Mwakasege amewataka wateja wa mkoa huo kupiga simu namba  0756 251 753 kwa ajili ya kupata msaada pale inapotokea tatizo wakati wa kufanya maboresho.

Nao wateja  wakiwemo Amina Ally pamoja na Nduguru John  wamepongeza huduma bora inayotolewa na TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini ikiwemo kufika eneo la tukio kwa ajili ya kuwasaidia  kufanya maboresho ya mfumo wa luku  pamoja na kutoa elimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *