NCHI 45 KUSHIRIKI MAONESHO YA NANE NANE 2024

0

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Bw. Nyasebwa Chimagu amewaomba Watanzania wanaoshughulika na kilimo kwenye mnyororo mzima wa thamani wasikose nafasi ya kushiriki katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nane Nane 2024 kwa sababu ni mwelekeo wa kukuza uchumi na kupanua mtandao mzima wa uzalishaji.

Bw. Nyasebwa ameeleza hayo leo Julai 22, 2024 wakati akihojiwa na Vyombo vya Habari, jijini Dodoma na kuongeza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alishaielekeza Wizara ya Kilimo kuhakikisha kuwa Maonesho haya yanakuwa ya taswira ya Kimataifa ambapo kwa mwaka huu yatafanyika katika Kanda Saba, huku Dodoma kufanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni.

Ameongeza kuwa wadau mbalimbali watashiriki ambap vijana na wanawake wanahamasishwa kuonesha namna gani wanazalisha, wanapata mitaji kwani kilimo kinalipa na ni biashara.

“Kwenye Nane Nane kutakuwa na ushindanishaji wa wakulima kuona teknolojia, mbinu, ujuzi na maarifa katika kilimo chao. Kutakuwa na vigezo ambapo wakulima wanatembelewa kuona wamefanya nini, uwekaji wa kumbukumbu za uzalishaji, namna anavyopata faida, namna anavyo tafuta masoko. Tuzo na zawadi zitakazotolewa kwa washindi zitaongeza ari ya wakulima wengi kuendelea kuboresha kilimo chao,” ameeleza Bw. Nyasebwa Chimagu.

Imeelezwa kuwa maandalizi ya mabanda yanaendelea, lakini pia teknolojia mbalimbali za uzalishaji wa mazao ya kilimo pamoja na mifugo vinaendelea kupangwa.

Naye Bi. Upendo Mndeme, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Huduma za Ugani amesema hadi sasa nchi 45 zimeonesha nia ya kushiriki maonesho chini ya uratibu wa pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili wageni wapate huduma stahiki. Amesema wageni wengine wamejisajili kwa ajili ya kupata maeneo ya kuonesha bidhaa na teknolojia.

“Wananchi wetu wana fursa ya kupata teknolojia kutoka kwa wenzetu na sisi waratibu tutapata kitu kipya kutoka kwa wenzetu kwa ajili ya kuboresha Maonesho haya ili yaweze kuleta tija kwa wakulima,” amesema Bi. Upendo.

Bi. Upendo amesema kuwa viwanja vya Nane Nane kila baada ya maonesho ya kila mwaka vitabaki kuwa Vituo Mahiri vya Kuhaurisha Teknolojia na Serikali imeanza ukarabati wa kuviendeleza viwe vya Kimataifa ili wakulima waendelee kujifunza teknolojia mpya za kilimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *