USALAMA WA MTANDAO NI MUHIMU KWA TAIFA -NAIBU WAZIRI MAHUNDI
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema suala la usalama wa kimtandao ni muhim ili kuhakikisha upatikanaji wa taarifa, huduma na bidhaa za mtandaoni ni salama na hazimuathiri mwananchi na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa ziara yake makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) tarehe 18 Julai, 2024 Mhandisi Mahundi ameishukuru timu zima ya TCRA kwa umahiri mkubwa katika usimamizi wa sekta hasa katika eneo la usalama mtandao.
Amesema, umahiri wa TCRA kunaifanya Wizara kuonekana inawajibika na kuendelea kulipa Taifa heshima huko duniani ambapo mpaka sasa tupo katika nafasi nzuri kimataifa katika masuala ya usalama mtandao.
Aidha, ametoa rai kwa TCRA kuendelea kukimbizana na mabadiliko ya teknolojia kwa wataalam kujifunza na kuongeza ujuzi mara kwa mara ili kuweza kukabiliana na wahalifu wa mtandaoni wanaoenda sambamba na kasi ya ukuaji wa teknolojia kwa kubuni mbinu mpya za kufanya uhalifu.
Mhandisi Mahundi amesema kuwa lengo la ziara yake ni kujifunza utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kumsaidia Mhe. Waziri Nape Nnauye ipasavyo lakini pia kuitendea haki nafasi adhimu aliyopewa na Mhe. Dkt. Samia ya kuwahudumia watanzania.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Kuwe amekiri kuwa teknolojia inavyokuwa wahalifu pia hutafuta mianya na mbinu mpya za kufanya halifu ambapo amebainisha chanzo cha matukio ya uhalifu mtandaoni yanasababishwa na watu wenyewe kwa ukosefu wa maadili kuliko teknolojia.