HUDUMA KWA WATEJA WA KILIMO KUTINGA NANE NANE 2024
Wateja na wadau mbalimbali wa kilimo wanakaribishwa kupata huduma kwa wateja inayotolewa na Wizara ya Kilimo ambapo timu yake itatinga katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nane Nane 2024.
Bw. Zacharia Gadiye, Mratibu Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Wizara ya Kilimo ameeleza kuwa “Wizara imejipanga kuhakikisha taarifa za sekta zitapatikana ili kuwezesha wakulima na wadau kupata elimu ya kilimo cha kisasa, teknolojia katika kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao.”
Amezungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari tarehe 17 Julai 2024 katika Ofisi za Wizara ya Kilimo, jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa pamoja na uwepo wa wataalam wa ugani katika ngazi za vijiji na kata, Wizara ya kilimo imefanya juhudi za kuimarisha mawasiliano kati ya mkulima na wataalam kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call Center). Huduma hizo zinapatikana kwa kupiga simu namba 0733 800200 au 0800 110810.
Maonesho ya Nane Nane 2024 yatafanyika Kitaifa Mkoani Dodoma katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma kuanzia tarehe 1 Agosti hadi 08 Agosti 2024. Aidha, huduma hiyo itapatikana pia kwa mawasiliano ya simu kwa wateja wa ndani au nje ya nchi.