MAONESHO YA NANENANE 2024 KUONGEZA WIGO WA SOKO LA MAZAO YA KILIMO
Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane 2024) yatasaidia kukuza mahusiano ya kibiashara na kutanua wigo wa soko la mazao ya kilimo na bidhaa za kilimo ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na ushiriki wa wadau mbalimbali wa kisekta.
Hayo yameelezwa na Bw. Mohamed Chikawe ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti katika Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Kilimo alipozungumza kwenye moja ya kituo cha Radio Jijini Dodoma tarehe 15 Julai, 2024.
“Maonesho ya kimataifa ya Nanenane yatafungua fursa za masoko ya bidhaa zetu na kuongeza ushirikiano wa kimataifa na nchi mbalimbali katika Sekta ya Kilimo, jambo litakalosaidia kutanua wigo wa kimasoko na kutatua changamoto mbalimbali kwenye kilimo hususan katika mabadiliko ya tabianchi, upatikanaji wa mbegu bora na kufanya utafiti ili kuweza kutatua changamoto hizo pamoja na kusaidiana katika uzalishaji” amesema Bw. Chikawe.
Bw. Chikawe amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na menejimenti ya Wizara ya Kilimo kwa kuonesha nia ya dhati katika kukuza Sekta ya Kilimo hivyo wakulima watumie fursa hiyo kufanya kilimo cha kisasa na wadau mbalimbali wawekeze katika Kilimo kwa kuwa kilimo kina fursa nyingi za biashara zinazoweza kuinua Pato la Taifa na mwananchi mmoja mmoja.
Aidha Bw. Chikawe ametumia jukwaa hilo katika kuwakaribisha wadau mbalimbali wa kilimo pamoja na wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo na kiwasisitiza kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo kuanzia tarehe 1-8 Agosti 2024 ili wajionee mapinduzi makubwa katika Sekta ya Kilimo.