TANESCO KINONDONI KUSINI WATOA ELIMU YA MABORESHO YA MFUMO WA LUKU

0

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kinondoni Kusini limetoa elimu ya maboresho ya mfumo wa mita za Luku kwa wateja wake wakiwemo wananchi na  wafanyabiashara  wanaokoboa nafaka mbalimbali ikiwemo Mahindi na Mpunga  katika Soko la Tandale na Mazense.

Akizungumza Julai 12, 2024 wakati akitoa elimu   ya maboresho ya mfumo wa Luku kwa wateja katika Kata ya Tandale na Mazense, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini Bi. Samia Chande, amesema kuwa lengo ni kuhakikisha wateja wanakuwa na uelewa mkubwa wa maboresho mfumo wa mita za  luku unaotarajiwa kufanyika kuanzia Julai 22, 2024.

Bi. Chande amesema kuwa kutokana na umuhimu wa maboresho ya mfumo wa luku wameona ni vizuri kutoka Ofisini na kuwatembelea wateja wao ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi.

“Tumewaelimisha taratibu za kufata ili waweze kufanya maboresho ya mfumo wa luku pamoja na kuwapatia mawasiliano yetu : namba ya simu ya mkoani 0756 251 753 ili watakapopata changamoto tuweze kuwafikia kwa haraka” amesema Bi. Chande.

Amesema kuwa utaratibu wa kutoa elimu kwa kuwafikia wateja  maeneo yao ni sehemu ya utaratibu wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Bi. Chande amesema kuwa lengo la maboresho ni kuzijengea uwezo mita za luku ziweze kuwa na ufanisi ambapo mteja atapewa tarakimu zenye makundi matatu na kuingiza katika luku yake kwa ajili ya maboresho.

Afisa Mkaguzi TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini Bw. Enock Emmanuel pamoja  Afisa Huduma kwa Wateja katoka Mkoa huo Bw. Jimmy Luberty wamesisitiza umuhimu wa wateja kufanya maboresho ya mita za luku ili kuleta tija katika upatikanaji wa huduma ya umeme.

Nao wateja  wakiwemo Bw. Abdallah Kombo pamoja na Bi Neema Moshi wamepongeza huduma bora inayotolewa na TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini ikiwemo kuanzisha utaratibu wa kuwatembelea kwa ajili ya kutoa elimu, kusikiliza changamoto zao, huku wakitoa wito utaratibu huo uwe endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *