MBUNGE MAVUNDE ALITAKA JIJI LA DODOMA KUKAMILISHA UPIMAJI NZUGUNI B

0

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh.Anthony Mavunde amelitaka Jiji la Dodoma Idara ya Ardhi kusimamia ukamilishaji wa zoezi la upimaji na umilikishaji ardhi katika Mtaa wa Nzuguni B Kata ya Nzuguni Jijjni Dodoma ambapo mpaka sasa ni asilimia 50 ya viwanja 12,000 ndio imepimwa na kuwataka kumalizia idadi iliyobaki.

Mavunde ameyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara wa wananchi wa kusikiliza kero za wananchi uliofanyika Jijini Dodoma.

“Ninaupongeza uongozi wa Jiji la Dodoma chini ya Mkurugenzi wa Ndg. John Lipesi Kayombo kwa namna ambavyo wameendelea kushughulikia migogoro mbalimbali ya Ardhi kwa kushirikiana kwa ukaribu na wizara ya Ardhi.

Zoezi la Upimaji wa Mtaa wa Nzuguni B limekuwa la muda mrefu na hivyo kupelekea ucheleweshwaji wa huduma za msingi za jamii na ufunguaji wa barabara.

Kazi hii ya upimaji ipo ndani ya uwezo wenu hakikisheni kuanzia mwishoni mwa mwezi huu saba mnaanza mchakato wa kumalizia upimaji na umilikishwaji kwa maeneo yaliyobaki ili tutatue kero hii kubwa kwa wananchi wa Nzuguni B” Alisema Mavunde

Katika wakati mwingine Mbunge Mavunde ameutaka uongozi wa Jiji la Dodoma kuangalia upatikanaji wa eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Soko na Shule ya Msingi mpya ambayo Mbunge Mavunde ameahidi kuchangia darasa moja la Tsh 20,000,000 ili kusogeza huduma za jamii kwa ukaribu.

Naye Diwani wa Kata ya Nzuguni Mh. Alloyce Luhega ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara ya lami na ujenzi wa madaraja ambayo ilikuwa kero kubwa hapo awali na pia kutumia fursa hiyo kumshukuru Mbunge Anthony Mavunde kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa katika utatuzi wa kero za wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *