SERIKALI ITAENDELEA KUSIMAMIA, KUKUZA UADILIFU WA MAADILI – DKT. BITEKO
Serikali itaendelea kusimamia na kukuza uadilifu wa maadili kama msingi wa maendeleo endelevu kupitia Sera na Sheria bora kwa kushirikisha wadau wa kidini, elimu, na jamii ili kuendeleza utamaduni ambapo maadili yatajumuishwa katika kila sehemu ya maisha ya Watanzania.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko katika uzinduzi wa Kitabu kiitwacho “MMONYOKO WA MAADILI NANI ALAUMIWE”, ambacho kimeandaliwa na kuandikwa na Mhe. Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally Mbwana, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Julai 3, 2024 BAKWATA Makao Makuu jijini Dar es Salaam.
“Kwa kukuza misingi ya uaminifu, haki, uadilifu, uwajibikaji, umoja wa kijamii, na ustawi endelevu. tutahakikisha kuwa safari ya maendeleo ya Tanzania inabaki imara katika maadili yetu ya thamani, pamoja na mustakabali ambao vijana wetu watarithi Taifa lenye uadilifu na fursa,” amesema Dkt. Biteko
Pia, amezihimiza taasisi za kidini nchini ikiwemo dini ya Kiislamu kushirikiana na Serikali katika kutoa mwongozo wa kiroho na mafundisho ya maadili kwa jamii katika kukabiliana na mwenendo hasi na kukuza tabia chanya.
“Qur’an inasisitiza umuhimu wa uaminifu, haki, na huruma katika maisha yote. Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wenye kutoa ushahidi kwa haki. Wala uadui wa watu usikupeleke kutowafanyia uadilifu. Fanyeni uadilifu, hivyo ndio kuwa karibu na uchamngu,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko ameiagiza Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kushirikisha wadau, kuhakikisha inahamasisha ushiriki wa familia katika malezi bora na ya kimaadili, kushiriki kikamilifu kulinda maadili katika jamii zetu kukuza uhusiano imara ndani ya familia na kukuza mafundisho ya maadili ndani ya kaya ili jamii itakuwa imara.
Vile vile, Sekta ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ihakikishe kwamba ndani ya taasisi za umma na Serikali, inaongoza kuwa mfano bora kwenye jamii juu ya maadili.
“Tuhakikishe tunatunga Sheria na Sera zitakazosimamia haki, usawa, na mienendo mema. Lakini pia tuwekeze katika programu zinazosaidia kukuza na kusimamia mienendo ya watumishi wa uma hasa vijana ambao ndiyo tegemeo kubwa la Taifa letu,” ameongeza Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine, amesisitiza kusimamia hoja ya maadili katika mtaala wa elimu, hasa kupitia taasisi za elimu, na kuhakikisha mtaala siyo tu unawapa wanafunzi maarifa bali pia uwajengee maadili ya uwajibikaji, heshima, na utii wa sheria.
Amesisitiza kusimamia hoja ya maadili katika mtaala wa elimu, hasa kupitia taasisi za elimu, na kuhakikisha mtaala siyo tu unawapa wanafunzi maarifa bali pia uwajengee maadili ya uwajibikaji, heshima, na utii wa sheria.
Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Ally Bin Mbwana amesema kitabu hicho kitasaidia sana katika kujenga, kusimamia na kukuza maadili kwa Watanzania. Amewataka kukitumia katika malezi ya jamii nzima hususan katika familia.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema wizara anayoisimamia itatumia kitabu hicho kama rejea katika machapisho yanayolenga kukemea ukiukaji wa maadili nchini.
Naye, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi, Hamad Yusuf Masauni amesema umefika wakati kwa jamii kujitafakari na kuchukua hatua.
“Siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa za kutekwa kwa baadhi ya watu na taarifa zao kuchapishwa kupitia vyombo vya habari na kuongeza kuwa Jeshi la polisi limefuatilia matukio yote ya uhalifu hatua zimechukuliwa,” amesema Mhandisi Masauni.
Uzinduzi huo wa Kitabu umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiislamu kutoka mikoa mbalimbali nchini.