VIJANA 175 WA UVCCM LUDEWA WAHITIMU MAFUNZO
Vijana zaidi ya 175 wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe (UVCCM) wamehitimu mafunzo ya uongozi na ujasiliamali yaliyotolewa na wakufunzi mbalimbali kwa muda wa siku 10 huku wakiacha alama kwa kufyatua tofali zaidi ya elfu 25,000 kwaajili ya uboreshaji majengo ya shule ya sekondari Masimbwe inayomilikiwa na CCM kupitia jumuiya ya wazazi.
Akihitimisha mafunzo hayo mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Njombe Samwel Mgaya amesema mafunzo hayo ni chachu kwa vijana katika kujitegemea huku akiitaka Idara ya maendeo ya jamii kuwapa kipaumbele vijana hao katika kupatiwa mikopo Ili waweze kujikwamua kiuchumi badala ya kuwayumbisha na kuwatolea kauli zisizofaa.
Naye mwenyekiti wa vijana Wilayani humo Ocol Haule amesema vijana hao waliopatiwa mafunzo ni kutoka katika vijiji vyote vya Wilaya ya Ludewa ambapo matarajio Yao ilikuwa kukusanya vijana zaidi ya 360 lakini waliofanikiwa kufika ni vijana 175.