WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI WAPATA ELIMU YA UTUNZAJI MAZINGIRA

0

Wachimbaji Wadogo wa Madini wamepatiwa elimu kuhusu  Utunzaji wa Mazingira pamoja na matumizi sahihi ya kemikali hususan Zebaki.

Elimu hiyo ilitolewa Juni 22, 2024 na Meneja  kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Bw. Gerald Meliyo Mollel pamoja na Mratibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ( NEMC)  Befrina Igulu  kwenye  Wiki ya Madini inayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Center Jijini Dodoma.

Akizungumza na wachimbaji wa Madini Meneja kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu Bw. Gerald Mollel alisema Zebaki ni moja ya kemikali hatari  kwenye mwili wa binadamu ambayo inaingia mwilini kwa njia ya hewa ambapo wachimbaji wa madini huitumia katika uchenjuaji wa madini.

Alisema kemikali nyingi hazitoi harufu hivyo huwa ngumu kubaini kuwa unavuta hewa yenye kemikali na pia kemikali inaingia mwilini kwa kuvuta hewa, mguso wa ngozi pamoja na kula au kunywa.

Mollel aliyataja  madhara ya matumizi yasiyo sahihi ya zebaki kwenye mwili wa binadamu kuwa ni pamoja kuharibu mfumo wa fahamu, kusababisha magonjwa ya kifua, kusababisha ulemavu wa kudumu na hata  kufa, pamoja na kusababisha magonjwa ya saratani, kuathiri mfumo wa uzazi na mfumo wa fahamu, kupoteza kumbukumbu pamoja na kuathiri na kusababisha  chembechembe za urithi.

Hata hivyo, Mollel alielezea namna ya kuepuka athari za kemikali ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa kinga sahihi muda wote utumiapo kemikali, kuwa na kisanduku cha huduma ya kwanza pamoja na kuwa na kadi ya usalama wa kemikali.

Aidha,  Mollel aliwataka wachimbaji wa madini kutumia njia sahihi za uchimbaji na uchenjuaji wa madini kwa kutumia njia mbadala iliyotolewa kwa kuepuka athari zitokanazo na matumizi ya zebaki.

Kwa upande wake, Mratibu wa Miradi kutoka NEMC  Dkt. Befrina Igulu alisema miradi yote ya uchimbaji chini ya Sheria ya mazingira inapaswa kufanya tathmini ya athari na kufanya ufuatiliaji wa vichafuzi.

Aliongeza kwamba,  sababu za uchafuzi wa mazingira ni wachimbaji wadogo kutokuwa na ufahamu sahihi kuhusu athari za matumizi ya  kemikali zinazotumika kwenye uchenjuaji, miongozo ya kutunza mazingira kusimamiwa na watu wasio kuwa na taaluma ya mazingira na madini.

Aidha,  Igulu alisema, baraza lina matarajio ya kuendeleza usimamizi wa kelele zitokanazo na shughuli za uzalishaji (krasha), usimamizi madhubuti na majitaka na taka ngumu kwa uchavuzi na hali ya hewa, umwagaji maji yenye sumu kwenye mazingira.

Igulu alisisitiza kwamba,  NEMC inasisitiza wadau kufanya kwa pamoja na taasisi zote za Serikali zinazohusiana na mazingira ikiwa ni pamoja na kufanya kaguzi za pamoja ili kuhifadhi na kulinda mazingira kwa ustawi wa maisha ya jamii.

Igulu aliongeza kwamba NEMC kwa kushirikiana na  Mamlaka Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Fedha wako kwenye majadiliano kuhusiana na kupunguza kodi kwenye vifaa mbala wa Zebaki ili kila mchimbaji aondokane na matumizi ya Zebaki.

Wiki ya Madini inakwenda Sambamba na Kongamano la Wachimbaji, mkutano FEMATA na Maonesho ya Madini na vifaa vya uchimbaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *