MADAKTARI BINGWA ZAIDI YA 450 KUTOA MATIBABU BURE, ARUSHA

0

Madaktari bingwa na watoa huduma za afya zaidi ya 450 kutoka kwenye Hospitali na Taasisi takribani 40 za afya nchini Tanzania wanatarajiwa kutoa huduma za vipimo na matibabu bure kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha kwa siku saba mfululizo kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo Juni 24, 2024.

Kauli hiyo imetolewa mapema leo Jumamosi Juni 22, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda mara baada ya kukagua maandalizi ya Kliniki hiyo ya afya inayotarajiwa kuzinduliwa Jumatatu ya wiki ijayo kwenye viwanja vya michezo vya Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.

Mkuu wa Mkoa ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi wote wa Arusha kujitokeza kwa wingi kwenye Kliniki hiyo, akitoa hakikisho la vipimo, matibabu na dawa bure kwa kila mwananchi atakaebainika na kugundulika kuwa na magonjwa na maradhi ya aina mbalimbali.

“Ndugu zangu asiwaambie mtu, kwenye suala la afya kuna watu wameuza nyumba zao, kuna watu wameuza viwanja, kuna watu wamefilisika biashara zao katika kupambana kuuguza ndugu zao na kuna nyakati nyingine kuna ndugu zetu wameshindwa hata kukomboa miili ya ndugu zao kutokana na madeni ya gharama za matibabu. Neema hii ambayo Mungu ametupa tukaitumie na mikono ya watumishi wa Mungu ikafungue baraka ili tukapate afya kupitia madaktari wetu hawa bingwa.” Amesema Mh. Makonda

Kulingana na Mkuu wa Mkoa Mhe. Makonda, Hospitali na Taasisi zitakazoshiriki kwenye kliniki hiyo na kutoa madaktari wake bingwa ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya afya ya akili Milembe, Hospitali ya kanda KCMC, Hospitali ya Kanda Benjamin Mkapa, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Taasisi ya mifupa Moi pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Hospitali ya Mawenzi, SAIFEE pamoja na hospitali na taasisi nyingine za ndani na nje ya Mkoa wa Arusha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *