WANANCHI WA BARIADI WAVUTIWA NA ELIMU YA FEDHA.
Baadhi ya wananchi wa Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha iendelee kuwapatia elimu ya fedha ikiwemo namna ya kutumia fedha, uwekaji akiba, uwekezaji, na umuhimu wa bima kutokana na wananchi wengi kuendelea kudidimia kiuchumi licha ya kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ujasiriamali na biashara.
Wakizungumza wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika shule ya msingi Bariadi Halmashauri ya Mji Bariadi mkoani Simiyu, baadhi ya wananchi hao walisema ukosefu wa elimu ya fedha umekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo yao ya kiuchumi huku wakiipongeza Wizara ya Fedha kwa kuendelea kutekeleza Mpango wake wa Kutoa Elimu ya Fedha nchi nzima.
‘’ Sasa hii ndiyo maana ya maendeleo ya kifedha, mnapotupatia elimu hii ya kifedha, hata kama ni mama aliye mzee unapompelekea elimu basi unatuinua kiuchumi ‘’ alisema Bw. John.
‘’Tunaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha ambayo imeweza kuja kutuwezesha elimu ya fedha, kuna watu wanakopa pesa na kushindwa kuelekeza kwenye kile alichokipanga, ikiwemo kununua nguo, na wengine kunywea pombe mwisho wa siku anafilisiwa‘’Alisema Bi. Witness
Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, alisema programu ya utoaji elimu ya fedha ni utekelezaji wa Mpango wa Wizara wa kutoa elimu hiyo nchi nzima ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya fedha ili waweze kujikwamua kiuchumi.
‘’Wizara ya Fedha imeona kuna haja na umuhimu wa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi, kwa hiyo ilitengeneza Mpango Mkuu wa Maendeleo wa miaka kumi, mpango huo umeanzia mwaka 2021 hadi 2030, ndani ya mpango huo kumeongelewa mambo mengi ikiwemo programu ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi’’alisema Bi. Mnzava.
Naye Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Mwile Kauzeni, alisema kuwa ni muhimu wananchi kutoa taarifa juu ya ukiukwaji wa sheria unaofanywa na baadhi ya watoa huduma za fedha wasio waaminifu, ili kuondoa changamoto wanazopata katika kupata huduma za fedha.
‘’Kuhusu mikopo umiza, Benki Kuu inaangalia na inatoa maelekezo kwamba hiyo mikopo umiza ifanywaje, kwa hiyo kama kuna mtu yeyote ambaye ameenda kukopa halafu akapata matatizo, tunaweza kuyasikiliza hapa tulipo, kwa sababu pia Benki Kuu tuna sehemu ya dawati la malalamiko, kwa hivyo mtu yeyote mwenye malalamiko kuhusiana na Sekta ya fedha anaruhusiwa kuuliza swali lolote” Alisema Bi. Kauzeni
Alisema kuwa elimu hiyo ya fedha ilianza kutolewa maeneo ya mijini kupitia maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kwa Mikoa ya Dar Es Salaam, Mwanza na Arusha, ambapo kwa sasa programu hiyo imejikita kuwafikia wananchi wote kwa lengo la kuwaongezea uelewa wa masuala ya Fedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika mahitaji na matumizi ya Huduma za Fedh.
Baadhi ya mikoa iliyofikiwa ni pamoja na Manyara, Singida, Kagera, Rukwa, Kigoma, na sasa ikiwa ni zamu ya mikoa ya Simiyu, Shinyanga, na Tabora ambapo mikoa yote nchini inatarajiwa kufikiwa.