SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA (NHC) LANUNUA RASMI ENEO LA URAFIKI

0

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limenunua rasmi eneo la Urafiki mapema mwaka huu, ikiwemo mali zote zilizokuwa chini ya Kampuni ya Urafiki wa Tanzania na China (Tanzania – China Friendship Textile CO LTD).

Meneja wa Mawasiliano kwa Umma wa  Shirika la Nyumba la Taifa ameyasema hayo leo wakati wa ziara ya kukagua maeneo mbalimbali ambayo sasa yatakuwa chini ya miliki ya NHC na kufafanua kuwa eneo hili linajumuisha nyumba, maghala, viwanja vya wazi, viwanda na mali nyinginezo.

Katika ziara yake, Saguya alielezea furaha yake na matumaini makubwa kuhusu hatua hii, akibainisha kwamba itasaidia kuboresha miundombinu na kuinua uchumi wa maeneo hayo na kuboresha mandhari ya jiji.

Amesema kuwa NHC, imelinunua eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 50 kutoka kwa mnada wa wazi kikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tatu.

Alisema kuwa, “Kupitia umiliki huu mpya, Shirika la Nyumba la Taifa limejipanga kuboresha maeneo haya ili kuendana na malengo yetu ya kutoa makazi bora na ya kisasa kwa wananchi. Tumeanza kwa kulipima eneo lote na kutambua mipaka yote inayolihusisha eneo hilo.

Eneo la Urafiki lina historia ndefu ya kuwa kituo muhimu cha viwanda na makazi, kikitoa mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania. Hivi sasa, NHC inapanga kufanyia maboresho makubwa eneo hili kwa kujenga miundombinu bora, nyumba za kisasa, na maeneo ya biashara ambayo yatavutia wawekezaji na wakazi wapya.

Shirika la Nyumba la Taifa linaamini kuwa mradi huu mpya utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa kwa ujumla, na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya makazi na maendeleo ya kiuchumi nchini. Katika mpango wa maendeleo ya NHC, eneo la Urafiki litawekewa mkazo maalum kwa ajili ya kuhakikisha kuwa linakuwa mfano bora wa maendeleo ya kisasa na endelevu.

Muungano alihitimisha kwa kusema, “Hii ni hatua muhimu kwa NHC na kwa taifa letu.

Tunawaomba wananchi na wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi zetu katika kuboresha na kuendeleza maeneo haya kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *