DUWASA KUWAFIKISHA MAHAKAMANI WADAIWA SUGU WA MAJI

0

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) inakusudia kuwafikisha Mahakamani wadaiwa sugu wote ndani ya siku Thelathini (30) kuanzia tarehe ya leo Mei 16, 2024.

Tamko hilo la DUWASA kwa Umma limetolewa leo Mei 16,2024 na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria Wakili Ayoub Mganda wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph.

“Kila mdaiwa sugu ameshapatiwa notisi ya kukumbushwa kulipa deni analodaiwa na muda wa ulipaji umekwisha na ikumbukwe DUWASA inatoa notisi hii kwa mujibu wa Kanuni ya 54 (2) ya Kanuni ya Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019”. Amesema Wakili Mganda

Aidha, wateja wengi hawakutumia fursa wala kuzingatia tangazo la ofa ya mwezi mmoja iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuanzia tarehe 25/03/2024 – 30/04/2024 ya wateja kurejeshewa huduma ya maji bila kulipia gharama ya urejeshaji shilingi 25,000/=.

Wakili Mganda amesema kitendo cha kufikishwa Mahakamani kitasababisha mteja kulipa gharama zote zitakazojitokeza katika uendeshaji wa kesi inayomkabili pamoja na usumbufu kwa Mamlaka.

DUWASA inaendelea kuwasisitiza wateja wote wanaodaiwa wafike Ofisi Kuu pamoja na Ofisi za Kanda zake ili kulipa madeni yao kwa makubaliano ya kimkataba ili kuepusha fedheha, gharama na usumbufu utakaojitokeza dhidi yao.

Kwa upande wake Meneja wa Ankara na Mdhibiti Madeni DUWASA, Philipo Funga amesema Mamlaka imefanya jitihada za ndani za kuwasitishia huduma wateja wote wenye madeni sugu kutokana na wateja hao kutoonyesha dhamira ya kulipa madeni yao na kupelekea Mamlaka kutangaza kusudio la kuwapeleka Mahakamani.

Wateja wapatao 5595 ambao wana madeni sugu ya kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 1.84 watafikishwa Mahakamani endapo hawatalipa madeni yao ndani kipindi cha siku 30 kuanzia leo.

Wateja 977 nje ya wanaodaiwa tayari wameshalipa madeni yao ya zaidi ya shilingi Milioni 148 kwa kutumia fursa ya Ofa ya Mhe. Rais.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *