DKT. KIDA, NA MKUU WA IDARA YA AFRIKA MASHARIKI YA UHOLANZI WAKUTANA NA KUJADILI SHUGHULI ZA UBORESHAJI WA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI NA BIASHARA
Mei 14, 2024, The Hague, Uholanzi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Afrika Mashariki wa Uholanzi, Bi. Sanne Lowenhardt pamoja na Mshauri Maalum kuhusu Africa wa Wizara hiyo Bw. Melle Leenstra kuhusu uboreshaji wa Mazingira ya Uwekezaji na Biashara.
Katika mazungumzo yao, Dkt. Kida alibainisha namna serikali ya Tanzania inavyoendelea kuchochea mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini kupitia falsafa ya ‘R nne’ iliyoasisiwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akitaja baadhi ya mageuzi hayo, Katibu Mkuu amesema kuwa pamoja na mambo mengine, eneo mahususi ni Maboresho ya Mazingira ya Uwekezaji na Biashara nchini ili kuvutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Uholanzi kwa kuwa ni mshirika muhimu wa Tanzania.
Wakitoa uzoefu wa nchi yao katika maboresho ya mazingira ya Uwekezaji na Biashara, Bi. Lowenhardt na Bw. Leenstra walimwambia Dkt. Kida kuwa, Uholanzi imefanikiwa kwa kuweka Mifumo, Sera na Mikakati mizuri inayotabirika na kuwafanya wawekezaji wawe na imani kwa serikali ili waamue kuwekeza.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. Balozi Caroline Chipeta aliishukuru nchi ya Uholanzi kwa kuendelea kuenzi Uhusiano wa kidiplomasia uliodumu kwa muda mrefu baina ya Tanzania na Uholanzi ambapo Tanzania imenufaika na mahusiano hayo katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Tanzania imeendelea kuimarisha mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kwa kuitambua na kuipa nafasi kwa kuwa ni wadau muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Itakumbukwa kuwa, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kupitia Kitengo chake cha Uboreshaji wa mazingira ya Uwekezaji na Biashara (BEU) inaratibu utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na Biashara (MKUMBI/ BLUEPRINT) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) kupitia mradi wa Business Environment Growth and Innovation BEGIN.
Dkt. Kida, alikuwa The Hague, Uholanzi, ambako akiamembatana na wataalamu mbalimbali kutoka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Wizara ya Fedha.