WATUMISHI WIZARA YA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO WAENDELEA KUTEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU KWA VITENDO

0

WATUMISHI wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wameendelea kutekeleza agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), la kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Mazoezi hayo yaliyohusisha michezo mbalimbali ikiwemo kuvuta kamba, mbio za polepole, mazoezi ya viungo, mpira wa miguu na netiboli yamefanyika leo Mei 11, 2024 katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma yakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa.

Akizungumza mara baada ya mazoezi hayo, Katibu Mkuu Gerson Msigwa amesema wizara hiyo ndio yenye dhamana ya kusimamia shughuli za michezo nchini hivyo, michezo ni moja ya kipaumbele chake.

Amesema watumishi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wanapaswa kuonesha mfano kwa kufanya mazoezi huku akisisitiza kuwa wizara hiyo inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha michezo kwa watumishi inakua endelevu na kuvutia wadau wengine kushiriki kwa kuwa michezo ni ajira, uchumi na furaha .

” Nawapongeza watumishi wa wizara, tangu tumetangaza utaratibu huu wa kufanya mazoezi kila Jumamosi wameitikia kwa nguvu, tunaunga mkono juhudi na maelekezo aliyoyatoa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa akizielekeza Taasisi za Serikali kushiriki kwa vitendo kwenye mazoezi na tunawakaribisha wengine kwenye mazoezi haya ya viungo” Amesisitiza.

Amesema wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya inaendelea kuandaa mpango mzuri wa kuwa na kampeni ya kuhamasisha mazoezi nchi nzima ili wananchi waweze kushiriki kufanya mazoezi ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Suleiman Serera amesema mazoezi yanasaidia kuongeza mshikamano, umoja, upendo na furaha mahala pa kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *