SERIKALI YA RAIS SAMIA KUCHIMBA VISIMA VYA MAJI KILA JIMBO LA KIJIJINI
Waziri wa Maji Nchini, Mhe. Jumaa Aweso amebainisha kuwa Dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kila jimbo la kijijini linapata visima vya maji safi na salama.
Waziri Aweso amelisema hilo leo tarehe 9 Mei, 2024 wakati akizungumza kwenye Bunge la Bajeti alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Akizungumza Bungeni, Waziri Aweso amesema :-
“Katika kuongeza kasi ya uendelezaji wa rasilimali za maji na utekelezaji wa miradi ya maji, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ilinunua mitambo 25 ya uchimbaji visima na seti 5 za mitambo ya ujenzi wa mbawawa.”
“Mwongozo wa matumizi ya mitambo hiyo umetolewa ili itumike kwa ufanisi na kuleta tija iliyokusudiwa. Katika mwaka 2023/24, Serikali kupitia mitambo hiyo imechimba visima 266 kwenye maeneo mbalimbali ya vijijini.”
“Vilevile, Serikali imefanya tathimini na kuandaa mpango wa kufikisha huduma ya maji kwenye vijiji ambavyo havina huduma ya maji ambapo jumla visima 900 vinatarajiwa kuchimbwa katika majimbo mbalimbali ya uchaguzi.”
“Hadi sasa kazi ya uchimbaji visima imeanza katika mikoa ya Kigoma, Manyara na Songwe na utafiti unaendelea kwenye mikoa mingine.”
” Kila jimbo la kijijini litachimbiwa visima. Narudia, kila Jimbo la vijijini litachimbiwa visima. Narudia tena, kila Jimbo la Vijijini litachimbiwa visima na asiyepata kisima atapata bwawa .” Asisitiza Waziri Aweso
” Wali wa kushiba, unaonekana kwenye sahani. Huu wali unatosha na tunasaza_ .” Alimalizia Waziri Aweso akizungumzia kuhusu uchimbwaji wa visima katika majimbo.