VIPAUMBELE VYA WIZARA YA MAJI MWAKA WA FEDHA 2024/2025
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema Wizara imeweka vipaumbele ambavyo vitazingatiwa katika mpango na bajeti ya mwaka 2024/25 ili kufikia lengo la kuwapatia huduma ya maji safi na salama kwa zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wa vijijini na zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wa mijini.
Vipaumbele hivyo ni kama ifuatavyo:-
1. Kuendelea na usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji
2. Kukamilisha utekelezaji wa miradi inayoendelea na kuendelea na ujenzi wa miradi mikubwa
3. Kuendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuongeza kasi ya uvunaji wa maji ya mvua kupitia ujenzi wa mabwawa ya ukubwa wa kati na mabwawa ya kimkakati kwa kushirikiana na Sekta za Mifugo, Kilimo, Utalii na Mazingira
4. Kuimarisha matumizi ya mitambo ya uchimbaji wa visima na mabwawa iliyonunuliwa ili kufikisha huduma ya maji kwenye vijiji ambavyo havina huduma ikiwa ni pamoja na kutekeleza Programu ya kuchimba visima 900 na ujenzi wa mabwawa madogo madogo
5. Kukamilisha uandaaji wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji (Water Master Plan), Mtandao wa Taifa wa Kusambaza Maji (National Water Grid) na kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002
6. Kupunguza upotevu wa maji kwa kuendelea kukarabati miundombinu chakavu, kufunga mifumo ya kuweza kutambua maeneo yenye mivujo (ILMS) na kushirikisha viongozi wa Serikali za Mitaa kwa ajili ya kutoa taarifa za upotevu wa maji kwa wakati
7. Kuongeza kasi ya ufungaji wa dira za malipo kabla ya matumizi ya maji (prepaid meters) ili kuongeza makusanyo na kupunguza malalamiko ya wateja
8. Kuongeza kasi ya uwekezaji wa miundombinu ya uondoshaji majitaka kwenye Miji Mikuu ya Mikoa na Wilaya
9. Kuimarisha utoaji wa huduma bora ya majisafi kupitia Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira na CBWSOs kwenye eneo la maunganisho ya wateja wapya na kuhakikisha masaa ya upatikanaji wa huduma ya maji yanaongezeka
10. Kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji na uendeshaji wa miradi na skimu za maji.