JESHI LA POLISI LAKANUSHA KUHUSIKA NA KIFO CHA BABU G

0

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa ya uongo na uzushi inayosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na kifo cha Robart Mushi @ Babu G. ambaye picha yake imeambatanishwa kwenye taarifa hizo kuwa alipotea tarehe 11 Aprili, 2024 na baadae kugundulika katika Chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Polisi Kilwa Road.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro amesema taarifa hiyo pia imedai kuwa Polisi kuhusika na kifo hicho kwa kumuua.

“Ukweli ni kwamba tarehe 11 Aprili, 2024 majira ya saa 10 Alfajiri Askari Polisi wa Usalama  barabarani alipewa taarifa na mwananchi kuwa eneo laTaa za kuongozea magari za Buguruni, Ilala  mtu mmoja mwanaume aliyekuwa akivuka  barabara eneo hilo la Kimboka kuelekea Chama aligongwa na gari ambalo halikusimama (hit and Run) .Mtu huyo alipata majeraha makubwa kichwani, kifuani na eneo la chini la mgongo na kisigino cha mguu wa kulia. Eneo hilo lina watu wengi ambao wanakesha kwa biashara mbalimbali na walishuhudia tukio hilo.” Amesema SACP Muliro.

Na kuongeza kuwa “Mtu huyo alipelekwa haraka hospitali ya Amana na Polisi  lakini baada ya kumfikisha Madaktari walibaini kuwa mtu huyo alikuwa tayari amekwishafariki, Kwa sababu chumba cha kuhifadhi maiti  cha hospitali ya Amana kilikuwa hakina nafasi, ilishauriwa akahifadhiwe kwenye Hospitali ya Jeshi la Polisi iliyo barabara ya Kilwa Temeke ambayo inatoa huduma hata kwa raia kuhusiana na suala hilo.Tarehe 21.4,2024  ndugu wa marehemu walipatikana na wakautambua mwili wa ndugu yao kwani hakuwa na kitambulisho wala simu. Taratibu za mwisho za mazishi zinafanywa ili akazikwe.”
 
Hata hivyo amesema kutokana na taharuki iliyotengenezwa na kujengwa kwa makusudi na mtu anayejiita Malisa gj na Bonoface Jacob ambao kwenye “post” zao walionesha nia ya wazi ya kutengeneza chuki dhidi ya Polisi na Serikali kwa  wananchi kuwa mtu huyo aliyepata ajali alikuwa ameuawa na Polisi.

Ameongeza kuwa kitendo kilichofanywa na watu hao ni kosa kisheria na hakivumiliki na lazima Jeshi lichukue hatua za kisheria dhidi ya wahusika ikiwa ni pamoja na kuwakamata , kuwahoji  kwa kina na kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo.

Amesema Jeshi la Polisi halitavumilia watu ambao wanaibuka na taarifa za uongo na uzushi ambazo zinalenga kujenga chuki na taharuki kwa wananchi. Jeshi litaendelea kusimamia misingi ya kisheria na halitakuwa na huruma kwa mtuhumiwa yoyote wa kihalifu na litamshughulikia haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *