MIAKA MITATU YA RAIS SAMIA NA MABADILIKO CHANYA SEKTA YA KILIMO DODOMA
Miaka 3 ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt, Samia Suluhu
Hassan imetajwa kuleta mabadiliko chanya katika eneo la kilimo ndani ya Jiji la
Dodoma kupitia matokeo makubwa yanayothibitishwa na wakulima, wafugaji pamoja na
wasimamizi wa masuala ya kilimo.
Akizungumza na vyombo vya habari Mkuu wa Divisheni ya Kilimo Mjini, Yustina
Munishi alisema kwa kipindi cha Miaka 3 ya serikali ya Awamu ya Sita, Jiji la Dodoma
limepiga hatua kubwa katika eneo la kilimo kutokana na uzalisahaji mkubwa wa mazao
ya chakula, mazao ya kibiashara halikadhalika ongezeko la mifugo.
Aidha, kupitia mazungumzo yake alisema “Serikali imekuwa na mchango mkubwa
kuyafikia mafanikio haya, kwakuwa wamekuwa kipaumbele kutoa fedha, usimamizi
mzuri, elimu kwa wakulima na watumishi, hii yote ni kuhakikisha kilimo cha Jiji letu
kinastawi siku hadi siku”
Munishi aliyataja na kuyafafanua maeneo mbalimbali katika Divisheni yake ambayo
yamekuwa na mafanikio yaliyotukuka kwa kipindi cha miaka 3.
Alisema zao la zabibu limekuwa ni moja ya zao la kimkakati ambalo linalimwa zaidi na
kwa mafanikio makubwa hadi sasa ndani ya Jiji la Dodoma kupitia msukumo na
hamasa iliyofanyika ikiwa ni pamoja na mafunzo mbalimnbali yaliyotolewa kwa
wakulima na watumishi kuhusiana na uzalishaji mzuri na wenye tija.
“Tumeongeza uzalishaji wa zao la Zabibu miche 113,306. Hadi sasa wakulima 500 na
watumishi 30 wameweza kupata mafunzo kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa
Kilimo Tanzania – Makutopora” alisema Munishi.
Aidha alisema kumekuwa naongezeko la viwanda zaidi ya 20 ambavyo vinaboresha na
kuongeza thamani ya zao la zabibu, ikiwa ni mafanikio waliyoyapata ndani ya miaka mi
tatu ya serikali ya awamu ya sita.
Sambamba na hayo alisema serikali imewasaidia kuboresha huduma za ugani kwa
kuwapatia vitendea kazi ikiwa ni pamoja na jumla ya pikipiki 28. Alisema pikipiki hizo
zimekuwa na msaada mkubwa katika kuboresha na kurahisisha huduma, kwakuwa
wakulima wengi wanafikiwa na kupata huduma za ugani na teknolojia mbalimbali, hali
inayopelekea ongezeko kubwa la uzalishaji wa chakula.
Hata hivyo alisema kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais. Dakt, Samia Suluhu Hassan,
divisheni ya kilimo mjini kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, wamehakikisha mbegu
ya alizeti ya ruzuku imetolewa kwa wakulima wote hadi wa ngazi ya Kata kwa bei nafuu.
“tumefanikiwa kununua na kusambaza mbegu ya alizeti ya ruzuku tani 45,000 zenye
thamani ya shilingi milioni 225 na kuziuza kwa wakulima kwa bei ya shilingi 5,000 kwa
kilo hali iliyowezesha kushuka kwa gharama ya mafuta ya alizeti kutoka (6,000 – 7,000)
kwa lita hadi sasa kufikia (4,000 – 5,000)” alisema Munishi.
Aidha alisema fanikio jingine walilolipata ni kusajili jumla ya wakulima 14,430 ambao pia
wameweza kupatiwa huduma ya kununua mbolea ya ruzuku.
“Awamu hii tumeweza kupata dozi 4,000 za madume bora ambayo yanapandishwa kwa
mitamba yetu na kuboresha uzalishaji kwa njia ya mirija” aliongezea Munishi na kusema
kuwa, kupitia teknolojia hiyo imepelekea ongezeko la maziwa na ngombe ambapo hadi
kufikia sasa mmfugaji mmoja anaweza kupata maziwa lita 20 – 30 kwa siku.
Aidha alisema kupitia ufugaji wa kuku, Divisheni ya kilimo Mjini ndani ya miaka mi tatu
ya Serikali ya Awamu ya Sita imeweza kupunguza vifo vya kuku kutoka asilimia 5
mpaka 3 kupitia utoaji wa chanjo uliofanyika.
Hata hivyo, alisema wamefanikiwa kuboresha miundombinu ya mifugo kwa kiasi
kikubwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa wigo katika minada mbalimbali hali ambayo
imesaidia kuhakikisha usalama wa mifugo isitoroshwe lakini pia kuondo mianya ya
upotevu wa ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo hayo.
Sambamba na hilo alisema eneo la Ipala wamefanikiwa kutengeneza bwawa la
kunyweshea mifugo linalowanufaisha zaidi ya wafugaji 1865 kwa Kata moja na pia
wananendelea kuboresha kwenye maeneo mengine yanayofaa kwaajili ya kutengeneza
mabirika hayo.
Aidha, alisema kwa kipindi cha miaka mi tatu cha Serikali ya Awamu ya Sita
wamefanikiwa kuchanja Ng’ombe 64,000, Mbuzi na Kondoo 52,340 kwa gharama nafuu
ya ruzuku.
“Divisheni yetu ipo kwa ajili ya kuwapa watu furaha na Lishe bora kwa sababu watu
wasipokula hawawezi kuwa na furaha. Watu wasipopata kuku na vitoweo kama nyama
ya ng’ombe hawawezi kupata furaha” Munishi aliongezea.
Kwa upande mwingine Munishi alisema kwa kipindi cha miaka mitatu halmashauri ya
Jiji imekuwa washindi wa kwanza kimkoa katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati
kwa mwaka 2023.
Munishi alihitimisha kwa kutoa shukurani pangezi za dhati kwa Rais. Mhe, Samia
Suluhu Hassan kwa kuboresha shughuli za kilimo katika Jiji la Dodoma na kuahidi
kuendelea kuunga mkono jitihada zake katika kuwaletea wanancghi maendeleo.