WATU 30 WANASWA NA POLISI KWA KUGHUSHI NYARAKA ZA NSSF
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na maofisa kutoka mfuko wa hifadhi ya jamii wa (NSSF) kwa nyakati tofauti kuanzia mwezi Desemba 2023hadi mwezi Aprili 2024 limewakamata watuhumiwa 30 kwa tuhuma za kughushi nyaraka mbalimbali zinazohusiana na mfuko wa hifadhi ya jamii wa NSSF kwa lengo la kujipatia malipo kwa njia ya udanganyifu kutoka kwenye mfuko huo.
Watuhumiwa hao wamekamatwa na nyaraka za bandia mbalimbali zinazohusu kuacha kazi, vyeti vya huduma, taarifa za uongo za ugonjwa, Hati za uongo za kufukuzwa kazi pamoja na fomu za kugushi za kuomba mafao ya NSSF.
Waliokamatwa ni na pamoja na, (1) Diocress Kahwa (35) mkazi wa Mbezi, mwalimu wa Shule ya Msingi Maxmilian ya Segerea (2) Barnabas Bonivencha na wenzake 11 wa kampuni binafsi ya ulinzi ya G4S waliowasilisha taarifa za uongo za kuacha kazi ili wapate mafao wakati bado wapo kazini.
Alikamatwa pia Gregory Rweikiza (44) mkazi wa Goba na Carolina Mushi (37) Mkazi wa Upanga, Ilala, mtumishi wa Benki ya Stanbink kwa tuhuma za kughushi taarifa za hospitali za ugonjwa za ili apate fao la matibabu. Waliokamatwa wengine ni Michael Mpogolo (38) na Sabato Thomas (27) wakazi wa Madale Mivumoni Dar es Salaam kwa tuhuma za kughushi nyaraka za wafanyakazi wawili marehemu (Servas Tesha na Korodias Shoo) waliokuwa wanafanya kazi katika Mgodi wa Geita (Geita Gold Mine).
Watuhumiwa wote watafikishwa Makahamani haraka iwezekanavyo kujibu tuhuma zinazowakabili, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawataka watu waachane na mambo ya udanganyifu au kughushi nyaraka kwani watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwafisha mahakamani kwa hatua za kisheria.