UZINDUZI WA KAULI MBIU NA NEMBO YA MIAKA 60 YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

0

Kuelekea maadhimisho ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Aprili 8 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua kauli mbiu inayosena “MIAKA 60 YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, TUMESHIKAMANA NA TUMEIMARIKA, KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU’’ pamoja na Nembo maalum itakayoenda kutumika katika maadhimisho hayo yatakayofanyika Aprili 26 katika uwanja wa uhuru Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo Aprili 8,2024 Jijini Dodoma Waziri mkuu amesema Muungano huo umeendelea kuwa na tija na kuchagiza maendeleo ya nchi na wananchi wote kwa ujumla.

“Kauli mbiu hii inatukumbusha kuwa Muungano wetu umekuwa kichocheo cha maendeleo kwa pande zote mbili za muungano, hakuna mwananchi ambaye hajafikiwa na faida za muungano wetu, ama kwa hakika Muungano wetu ni wa udugu, wananchi wengi wameunganisha udugu, urafiki na wengine wameoleana,”amesema.

Amesema pamoja na misingi ya kisiasa, hakuna anayeweza kuvunja udugu wa damu uliopo, Udongo ulianza kuchanganywa sasa kuna mchanganyiko mkubwa wa damu.

Pia amezitaka taasisi zinazotoa elimu, ziendelee kufundisha mada kuhusu muungano kuanzia elimu ya awali ili watoto na vijana waufahamu na wawe walinzi na hatimaye wawe vinara katika kuundeleza Muungano huo.

Aidha amesema uzinduzi huo wa Nembo na kaulimbiu ya Miaka 60 ni moja ya sehemu ya maadhimisho ambapo mwaka huu yamepambwa na matukio mengine muhimu ikiwemo uchaguzi wa wenyeviti wa mitaa hivyo amewaomba wananchi kuchagua viongozi wenye weledi na watakaoweza kudumisha Muungano.

Waziri Mkuu pia ametoa rai kwa wapigakura wote kuhakikisha wanajiridhisha na kushiriki taratibu za kuwafanya kuwa na sifa za kushiriki kuchagua Viongozi wenye uwezo na wenye nia njema na Muungano.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Juma amesema Muungano ni kitu muhimu na kila mtanzania analo jukumu la kuulinda.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amesema Muungano huo ni sawa na Jubelei ya almasi, hivyo, haina budi kukaa pamoja kama Taifa moja kumshukuru Mungu na kuiadhimisha kwa furaha miaka hiyo 60.

“Kuelekea maadhimisho hayo miradi ya maendeleo itazinduliwa na Viongozi Wakuu wa Kitaifa pamoja na Viongozi wengine wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri na Wakuu wa Mikoa, hivyo, niwaombe Waheshimiwa Mawaziri kushiriki ipasavyo katika uzinduzi wa Miradi mtakayopangiwa kuzindua ikiwa ni pamoja na kuambatana na Viongiozi wa Kitaifa katika uzinduzi wa miradi watakayoizindua,”amesema.

Ikumbukwe kuwa Tanzania inaenda kutimiza miaka 60 tangu kuundwa kwake baada ya Mataifa mawili kuungana kati ya Tanganyika na Zanzibar Aprili 26,1964 na kuwa Nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *