WAZIRI PROF. MKUMBO AWAONGOZA WATAALAMU WA WIZARA YAKE KUTOA SEMINA KWA KAMATI YA BUNGE
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.) akiambatana na Katibu Mkuu Dkt. Tausi Kida amewaongoza wataalamu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kutoa semina kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na Ofisi hiyo.
Katika semina hiyo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Maboresho ya Mazingira ya Uwekezaji na Biashara Bw. Baraka Aligaesha amefanya wasilisho kuhusu maboresho ya mazingira ya biashara katika Sheria, Kanuni, Tozo na Mifumo ya TEHAMA yaliyofanywa na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji.
Aidha, katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bw. Lawrence Mafuru akifanya wasilisho linalohusu mchakato wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Na Mkuu wa Idara ya Huduma na Ushauri wa Kimenejimenti kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Bi. Neema Musomba akifanya wasilisho ambalo pamoja na mambo mengine, liliangazia hatua zilizochukuliwa na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji katika kuunganisha mashirika ya Umma ili kuongeza ufanisi na tija kwa mashirika hayo.
Aidha, wajumbe wa kamati hiyo inayoongozwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama (Mb.), walipata wasaa wa kuuliza maswali na kupokea ufafanuzi kutoka kwa Mhe. Waziri, Katibu Mkuu na watalaamu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.
Dkt. Mhagama alihitimisha kwa kusema kuwa Kamati yake inavutiwa na namna Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji pamoja na taasisi zilizo chini yake zinavyofanya kazi.