“MA DAS NA MA-DED WENGI MNADHIBITI BIASHARA NA SIO KUWEZESHA” WAZIRI PROF. KITILA
Waziri Prof. Kitila awataka Makatibu Tawala na Wakurugenzi kuwezesha Ufanyikaji wa Biashara na sio kudhibiti.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amewataka Makatibu tawala na wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha wanashiriki kuwezesha kufanyika kwa Biashara katika mazingira yao ili Serikali iweze kukusanya kodi kwaajili ya kuendesha nchi bila kukwamisha wananchi au kuwakandamiza.
Ametoa Maagizo hayo leo 06 April, 2024 Jijini Dodoma wakati Akifungua Semina ya Makatibu tawala wa mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za mitaa kuelekea zoezi la ukusanyaji maoni ya wananchi na wadau katika Dira ya Taifa ya maendeleo 2050.
Amesema kumekuwa na changamoto katika Serikali za ndani katika suala la Biashara kwani wengi wamejikuta wakidhibiti na sio kuwezesha.
“Walipa kodi namba moja ni wafanyabiashara, ili tupate mishahara yetu ni lazima kodi zilipwe, ili kodi zilipwe lazima biashara ifanyike, lazima tuweke mazingira ya kufanya biashara, Makatibu tawala na wakurugenzi ni lazima ujiulize katika majukumu yako ni kwa kiasi gani unashiriki kuwezesha kufanyika kwa biashara.na kwa kiasi gani mnashiriki katika kukwamisha Biashara, unapokwamisha biashara unakwamisha upatikanaji wa kodi, ukikwamisha upatikanaji wa kodi unakwamisha upatikanaji wa mishahara kwa watumishi wa Umma” amesema Prof. Kitila
Ameendelea kusisitiza iwapo watakuwa wanachangia kukwamisha Biashara ndivyo wanachangia kuhatarisha usalama wa Nchi kwani ikitokea watumishi wa Umma wanakuwa hawana utulivu basi na Serikali haiwezi kuwa na utulivu
“ukikwamisha biashara ukakwamisha kodi, unakwamisha uwezo wa Serikali kuhudumia wananchi wake”
Amesema katika maeneo mengi kumekuwa na changamoto ikiwemo wafanyabiashara wanapokwenda kukaguliwa Leseni wanachofanyiwa ni kudhibitiwa mfano kulazimishwa kufunga biashara jambo ambalo sio uwezeshaji wa Biashara kufanyika.
“wengi wenu bado ni wadhibiti wa Biashara, sio wawezeshaji wa Biashara” Waziri Prof. Kitila
Aidha, Waziri ameonesha kukerwa na kutoza Ushuru kwenye kila Vituo vya Mabasi pale yanapokuwa yanasafiri kwani hutakiwa kulipa tozo kwa kila Halmashauri wawapo katika safari jambo ambalo ametaka kutengenezwa kwa utaratibu mzuri wa ulipaji tozo ili kuepusha usumbufu
“Kwani nyie hamuwezi kukaa Makatibu tawala wa Mikoa husika mkatengeneza utaratibu kwamba mtu anaweza akalipa kodi moja na nyie mkagawana, kwanini isiwezekane? kwanini kila akipita kwenye Kituo cha Basi akalipe, sisi ni Serikali na ndio Serikali moja” ameeleza Waziri Prof. Kitila
Amesikitishwa na kero hiyo ambayo ipo mpaka kwa wakulima ambao wanasafirisha mazao yao kwani wamekuwa wakikumbana na kadhia hizo hizo.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida amesema Wizara inatambua mchango wa wadau katika mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, hivyo kupitia Semina hiyo watapata uelewa kuhusu maandalizi ya Dira hiyo na kutambua umhimu wa kushirikisha makundi mbalimbali ya kijamii.
“Katika Kikao hiki mtapata semina ya uelewa kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 na kufahamu maeneo yaliyoainishwa kwaajili ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi katika maeneo yao na nyenzo mbalimbali zitakazotumika katika ukusanyaji wa maoni hayo.” Amesema Dkt. Kida
Ikumbukwe kuwa Tukio hilo lililofanyika leo ni mwendelezo wa Programu iliyopangwa ya kuhabarisha Viongozi mbalimbali katika maandalizi ya Mchakato wa Dira ya maendeleo ya Taifa 2050.