WATEJA DUWASA WAFURAHIA OFA YA SIKU 30 YA RAIS SAMIA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeendelea kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa Machi 23, 2024 kupitia kwa Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb) la kuwarejeshea huduma ya maji wateja waliyositishiwa huduma hiyo bila kulipa pesa ya kurejeshewa huduma ya maji kwa muda wa siku thelathini kuanzia Machi 25, 2024 hadi Aprili 30, 2024, ambapo mteja atawajibika kulipa deni analodaiwa kwa awamu kulingana na makubaliano na Mamlaka husika.
DUWASA inawahimiza wateja wake wote waliyositishiwa huduma ya maji kwa kutolipa ankara zao kwa wakati kufika katika Ofisi za DUWASA Makao Makuu na katika Ofisi za Kanda za Miji ya Bahi, Chamwino, Kibaigwa na Kongwa ili waweze kurejeshewa huduma na kuweka makubaliano ya kulipa madeni yao.
Zaidi ya wateja 250 wa Jiji la Dodoma na Kanda zake zote Nne wamerejeshewa huduma ya maji kuanzia Machi 25, 2024 hadi sasa na Jumla ya Shilingi Milioni 33.05 zimekusanywa ikiwa ni madeni ya wateja bila faini ya kurejeshewa huduma maji.
Baadhi ya wananchi waliyorejeshewa huduma ya maji katika Jiji la Dodoma wamemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wake kuwapatia huduma muhimu ya majisafi.