RAIS SAMIA AMETUHESHIMISHA NA KUTUFANYIA MAKUBWA WANAWAKE ASIBEZWE- DITOPILE

0

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mariam Ditopile, amesema miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imekuwa na manufaa makubwa kwa wanawake wa Tanzania.

Amesema miongoni mwa mambo ya kujivunia katika kipindi hicho ni pamoja na kuimarishwa kwa huduma za kijamii zinazomgusa mwanamke moja kwa moja na kusaidia kutatua changamoto zao.

Ditopile ameeleza hayo leo Machi 25,2024 alipozungumza na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine alijibu hoja za upotoshaji ukweli kuhusu uondgozi wa Rais Samia kuhusu kuwainua wanawake nchini.

“Ndani ya Kipindi kifupi cha Rais Samia ametuheshimisha wanawake kwa kuboresha huduma za ustawi wa jamii, kuchochea maendeleo ya Jinsia na uwezeshaji wa wanawake, kuimarisha upatikanaji wa haki na Maendeleo ya Mtoto, pia ameimarisha utekelezaji wa Mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

“Rais Samia ni Kinara wa utekelezaji wa eneo la Haki na usawa wa kiuchumi kwa Wanawake na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza na kushiriki kwa vitendo Programu ya Kitaifa ya utekelezaji wa Ahadi za Nchi kuhusu Kizazi chenye usawa 2021/2022-2025/2026 (Generation Equality Forum Commitments), alisema.

Alieleza kuwa utawala wa Rais Dk. Samia umeongeza kazi zenye staha kwa kuendeleza biashara na urasimishaji wa biashara za wanawake, Rais Samia ameboresha upatikanaji na matumizi ya teknolojia nafuu na zinazofaa ili kuongeza Uwezo wa wanawake wa kuzalisha bidhaa zenye Ushindani wa Soko la ndani na nje.

“Tumeshuhudia chini ya Utawala wa Rais Samia akianzisha na kuendeleza vituo vya malezi na makuzi ya watoto, ameongeza uwekezaji katika Usambazaji wa Maji, umeme na Nishati Mbadala yenye kutunza mazingira na matumizi ya teknolojia yenye gharama nafuu na inayofaa kwa kutatua changamoto za majukumu mengi kwa Wanawake katika maeneo ya vijijini na Mijini.

“Rais Samia ameongeza uwekezaji katika Programu za Elimu kwa wasichana, ameimarisha afua zinazoongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika Kumiliki, Kusimamia na kufaidika na Ardhi na rasilimali nyingine za uzalishaji na ameongeza wigo wa utoaji huduma kwa familia kupitia mifuko ya Hifadhi ya jamii,” alieleza.

Kwa mujibu wa Ditopile, Rais Samia katika kuhakikisha kuwa haki za wanawake na hasa wajane zinapatikana hapa nchini Kampeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ambayo ni mojawapo ya afua za programu ya kizazi chenye usawa yenye lengo la kulinda na kukuza haki ya upatikanaji wa huduma za Msaada wa kisheria Nchini

Alisema kuwa Wa Tanzania ni mashuhuda jinsi Wasichana wenye ufaulu wa juu wamefadhiliwa kusoma masomo ya utabibu, uhandisi, Sayansi na Teknolojia na Hisabati kupitia Samia Scholarship.

“Hii inadhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha watoto wa kike kuingia katika Ushindani wa Soko la Ajira kwenye ulimwengu wa kidijitali na kuongeza wigo wa kuteuliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi na uamuzi,” alisema.

Aliongeza kuwa “Programu mbalimbali kama” Mtue Mama Ndoo kichwani ” na ile ya” Kumtua Mama Kuni Kichwani “zinaendelea kutekelezwa zikiwanufaisha wanawake wengi Mijini na Vijijini, hakika wanawake tunajivunia uongozi wa Rais Samia.”

Hivi karibuni moja wa wanagarakati wa muda mrefu nchini, Dk. Ananilea Nkya alinukuliwa akidai kuwa Rais Samia bado hajawasidia wanawake nchini kwa kuwa mchakato wa katiba mpya haujakamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *