WATUMISHI WA HALMASHAURI WATIWA HATIANI KWA KUOMBA NA KUPOKEA HONGO
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imewahukumu Bw. Nelson Mwakilasa ambaye ni msaidizi wa Mkuu wa Masoko na Felister Mwanisongole ambaye ni Askari Mgambo, wote hao wakiwa ni watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Watumishi hao wameamuriwa kulipa faini ya Shilingi 600,000/= kila mmoja au kwenda jela miaka mitatu kwa makosa ya kuomba na kupokea hongo ya Shilingi 75,000/=.
Hukumu hiyo dhidi ya Nelson Mwakilasa na Felister Mwanisongole katika shauri la jinai Na. 77/2023, imetolewa chini ya Mhe. Mtengeti Sangiwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mbeya, Machi 22, 2024.
Washtakiwa hao walishawishi, kuomba na kupokea hongo ya Shilingi 75,000/= kutoka kwa wafanyabiashara ili wawaruhusu wafanyabiashara katika Soko la Magorofani ndani ya jiji la Mbeya, kufanya biashara bila ya kuwa na leseni ya biashara.
Washtakiwa wamelipa faini na kuachiwa huru na mahakama imewaamuru washtakiwa warejeshe kiasi cha shilingi 75,000/= walichopokea toka kwa wafanyabiashara ili zirejeshewe kwa waathirika.