SAGINI ATAKA KUWEPO SHERIA YA KUWATAMBUA WANAOTUMIA NEMBO HALALI KATIKA VYAKULA

0

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) amesema kunahitajika kutungwa Sheria madhubuti ili wale wote wanaotumia Nembo Halali katika Vyakula au Vinywaji wawe wanathibitishwa na Taasisi zinazosimamia Viwango nchini kwa maslahi na ulinzi wa walaji wa Ndani na Nje ya Nchi.

Ameyasema hayo Machi 23, 2024 wakati akihutubia katika ufunguzi wa Kongamano la Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu nchini lenye Kauli mbiu isemayo;- “Uchumi Halali kwa Maendeleo ya Jamii” lililofanyika katika Ukumbi wa DYCC Chang’ombe Jijini Dar es Salaam, Mhe. Sagini alisema kuwa katika mchakato huo Serikali itashirikisha wadau mbalimbali kupitia Wizara yenye dhamana ya biashara, Afya na Wifugo, wanazuoni na wataalamu wa masuala ya Halali.

“Kama Serikali, tuna wajibu wa kutunga Sera na Sheria wezeshi kwa ajili ya Uchumi Halali ili kuweza kunufaika na matunda yake, juhudi hizo zimeanza miaka mingi katika maeneo mengi kwa mfano masuala ya uchinjaji wanyama juhudi zimekuwa zikifanywa tangu wakati wa ukoloni kuhakikisha kuwa misingi Halali katika machinjio ya serikali na baadhi ya binafsi yanazingatiwa kadhalika, kwa kutambua uwepo wa soko kubwa la nyama Nje ya Nchi, serikali inatambua uwepo wa taasisi ambazo inazitambuwa kutoa Halali Certification kwa nyama zinazosafirishwa katika masoko yanayozingatia misingi ya Halali” Alisema Naibu Waziri Sagini.

Sagini alisema kuwa, neno Halali linagusa maeneo mbalimbali ya maisha ya binadamu ikiwepo uchumi na uchumi Halali una nyanja nyingi na maeneo mengi kuanzia vyakula, vinywaji, madawa, taasisi za fedha, viwanda, biashara, mavazi, vipodozi, utalii, usafirishaji na bila kusahau utungaji wa sera na sheria zinazotambua uchumi huu muhimu duniani kama ambavyo tunatarajia kuelimika kutoka kwa watoa mada wetu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (HAY-ATUL-ULAMAA) Sheikh Abdullah Swaleh Ndauga, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa namna inavyofanya kazi kwa weledi, ambapo aliwataka wanazuoni kutumia kongamano hilo kutumia kauli mbiu ya Uchumi Halali kwa maendeleo ya Jamii kila wawapo ndani ya jamii kwani misingi ya uchumi wa kiislamu imejengeka katika biashara, kuunda na kusaidiana pia mwanadamu yeyote anahitaji sifa kama hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *