BIL. 35 KUJENGA JENGO LA KISASA LA KITUO CHA JEMOLOJIA JIJINI ARUSHA

0

Serikali kupitia Wizara ya Madini  inatarajia kutumia shilingi bilioni 35 kujenga jengo pacha la Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) jijini Arusha ambalo litasaidia kuongeza udahili kutoka wanafunzi 180 hadi 450 kwa mwaka.

Hayo yamebainishwa leo Machi 22,2024 na Kaimu Mratibu wa kituo hicho, Mhandisi Ally Maganga wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari  kuhusu mradi wa  ujenzi wa jengo hilo.

Mhandisi Maganga amesema, jengo hilo litakuwa na miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa, makumbusho, masoko ya madini ya vito, karakana za uongezaji thamani madini, maabara za madini ya vito na bidhaa za usonara, ofisi na mabweni ya wanafunzi.

Amesema, jengo hilo litakuwa mahsusi kwa utoaji wa mafunzo ya kuongeza thamani madini ya vito ,minada ya madini ya vito na maonesho ya madini.

Mhandisi Maganga ameongeza kuwa,  jengo litatimiza ndoto kubwa ya Serikali ya Tanzania kwa  kulifanya eneo hili kuwa  kitovu cha madini ya vito barani Afrika, hii ni kutokana na wingi wa rasilimali madini ya vito yaliyopo nchini.

Kuhusu miundombinu ya jengo hilo,Mhandisi Maganga ameeleza kuwa, ndani ya jengo hilo pacha kutakuwa na ofisi za Tume ya Madini pamoja na biashara ya  minada ya madini ya vito ambayo yatasaidia kuleta fedha za kigeni nchini.

Akielezea kuhusu hali ya teknolojia ya uthaminishaji, Mhandisi Maganga amesema kuwa,bado nchi za Afrika zina changamoto kubwa ya teknolojia ya kusanifu madini, hivyo TGC itakuwa mkombozi mkubwa kwa wadau mbalimbali wa madini ya vito na metali hususani katika kuchakata na uthaminishaji.

Mradi huu unatarajia kukamilika ndani ya miaka miwili ijayo baada ya taratibu zingine kukamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *