TFRA, WAZALISHAJI WA MBOLEA WAAZIMIA KUMALIZA UTEGEMEZI WA MBOLEA

0

Mamlaka ya Udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA), imekutana na kufanya mazungumzo na wazalishaji wa mbolea nchini ambapo wamejadili mustakabali wa tasnia ya mbolea wenye lengo la kupunguza uingizaji wa mbolea ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka, Joel Laurent wakati wa kikao baina ya TFRA na wazalishaji wa ndani wa mbolea kilichofanyika tarehe 20 Machi, 2024 katika ukumbi wa Mamlaka jijini Dar Es Salaam.

Amesema kupungua kwa utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchini kutapunguza matumizi ya fedha za kigeni na hivyo kuongeza mchango wa Sekta ya Kilimo kwenye Uchumi wa Taifa na kufikia asilimia 10.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho Mkurugenzi Laurent amesema, maono ya Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ifikapo 2030 ni kuhakikisha nchi inajitegemea kwa asilimia 100 katika kupata pembejeo ya mbolea kwa kutumia viwanda vya ndani.

Ameeleza kuwa ili kufikia azima hiyo, Mamlaka imekutana na wazalishaji wa ndani ili kujadiliana maeneo ya kufanyia kazi ili kuwawezesha kutatua changamoto wanazokabiliana nazo kutakakopelekea kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo na hivyo nchi kujitosheleza. 

Laurent amebainisha kuwa, Ili kufikia ajenda 10/30: Kilimo ni Biashara, juhudi zinafanyika ili kuongeza kiasi cha mbolea inayotumika kwenye hekta 1 kutoka kg. 19 mpaka wastani wa kilo 50 kwa hekta moja.

Amesema wastani wa mahitaji ya mbolea kwa mwaka ni takribni tani 848,000 kwa mbolea zote na kueleza kuwa matarajio ya Mamlaka ni kuongezeka kwa matumizi ya mbolea ifikapo 2030 kutakako tokana na uelewa wa manufaa ya kutumia mbolea kwenye kilimo, uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo kama zinavyoelekezwa na Maafisa Ugani wetu kayika maeneo yao, wakulima kuhamasishwa kutumia mbolea zinazozalishwa nchini pamoja na bei ya bidhaa hiyo kuwa himilivu kutakakopelekea kila mkulima kumudu gharama hizo.

Kwa upande wake, Tosky Hans Mkurugenzi Mtendaji wa Minjingu Mining and fertilizer, ameipongeza Mamlaka kwa kuitisha kikao kilichoangazia namna tasnia ya mbolea nchini inavyoweza kuongeza uzalishaji na utoshelevu kulingana na mahitaji ya nchi.

Amesema huu ni mwanzo mzuri na kuishauri TFRA kuyaingiza yote waliyokubaliana kwenye matendo ili yasaidie sana nchi katika kufikia azma ya kujitosheleza kwa mahitaji ya mbolea nchini na nchi jirani.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hapco Tanzania Limited, Conrad Massawe amesema, TFRA imekuwa ikishirikiana na wadau kwa muda mrefu na kuhakikisha mkulima anapata mbolea bora na kwa bei himilivu na kueleza kikao kilichofanyika kimekuwa na manufaa makubwa na kuomba moto ulioanzishwa na Mamlaka uendelee.

Wakati huohuo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Mbolea Itracom Nduwimana Nazaire amempongeza Mkurugenzi Laurent kwa juhudi anazozifanya katika kutatua changamoto za wazalishaji wa mbolea nchini na kueleza kikao hicho ni mwendelezo wa yaliyojadiliwa wakati wa ziara ya kiongozi huyo kwenye viwanda vya mbolea ncini na Itracom ikiwepo.

Amesema mpaka sasa kiwanda chake kina uwezo wa kuzalisha tani laki 8 na wanatarajia mpaka mwezi Juni watakuwa wamekamilisha ujenzi utakaopelekea kuzalisha kiasi cha tani milioni 1 kwa mwaka na kubainisha wako katika hatua za mwsho wa ujenzi wa kiwanda hicho.

Akitaja maazimio ya kikao hicho, William Ngereja Mjumbe wa Bodi ya Itracom alisema  ni pamoja na TFRA wakishirikiana na wazalishaji wa ndani wa mbolea kuja na sera, kanuni na sheria zitakazosaidia kulinda wazalishaji wa ndani wa mbolea, namna bora ya kufikisha mbolea kwa wakulima, namna bora ya kuboresha unufaikaji wa ruzuku ya mbolea inayotolewa na serikali, namna bora ya kuagiza mbolea zinazotoka nje kama malighafi kwa viwanda vya ndani na mwishowamepanga kukutana baada ya siku 7ili  kupata mrejesho wa maazimio waliyoyafikia katika kikao cha leo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *